149 wauawa kufuatia mapigano Hodeidah
12 Novemba 2018Wanaoiunga mkono serikali na wanaofadhiliwa na muungano wa Saudia Arabia wanapigana kuwaondoa waasi wa Huthi kutoka mji huo, ambao ni makaazi ya raia milioni 14 wa Yemen wanaokabiliwa na hatari ya njaa. Wakaazi na majeshi ya serikali wanasema waasi hao wamekita kambi katika mapaa ya nyumba mashariki ya mji wa Hodeidah.
Mratibu wa Shirika la Kuwasadia Watoto la Save the Children nchini Yemen, Mariam Aldogani, amesema raia eneo la Hodeidah wanaishi kwa woga. Akizungumza kwa njia ya simu na shirika la Habari la Ufaransa, AFP, mwishoni mwa wiki, Aldogani alisema mapigano bado yanaendelea huku mashambulizi yakisikika.
Jana Jumapili, Waziri wa wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alimshauri Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia, mshirika mkuu wa Marekani, kushiriki mazungumzo ya amani. Leo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Jeremy Hunt anatarajiwa kuzuru Saudi Arabia, ambapo atamshinikiza Mfalme Salman na mwanawe kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kusitisha mapigano nchini Yemen.
Marekani pamoja na Uingereza ni wafadhili wakuu wa silaha kwa Saudi Arabia. Mashirika ya misaada yameeleza hofu ya usalama kwa watu laki sita wanaoishi mjini Hodeidah, na mamilioni ya wengine wanaotegemea bandari kwa kufikishiwa chakula na misaada ya kibinadamu. Kulingana na takwimu za shirika la habari la Ufaransa, AFP, madaktari katika hospitali za mji huo wameripoti kuuawa kwa waasi 110 na watu 32 wanaoiunga mkono serikali katika mapigano yanayoendelea.
Waasi wameanza kuwaondoa wenzao waliojeruhiwa hadi mji mkuu Sanaa, ambao Wahuthi waliouteka mwaka 2014. Saudi Arabia pamoja na washirika wake waliingilia kati mapigano ya serikali ya Yemen dhidi ya Wahuthi mwaka 2015, na kuchochea kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro mbaya zaidi ya kibinadamu.
Takriban watu 600 wameuawa tangu mapigano kuzuka mjini Hodeidah Novemba Mosi mwaka huu wa 2018. Balozi wa Yemen katika Umoja wa Mataifa, Martin Griffins, anashinikiza kufanyika kwa mazungumzo ya amani kati ya Wahuthi na serikali kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mazungumzo ambayo yamekuwa yakiungwa mkono na Umoja wa Mataifa yamekosa kufanikiwa kupata suluhu ya mapigano nchini Yemen. Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa watu elfu kumi wameuawa katika mapigano hayo tangu mwaka 2015. Hata hivyo mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaamini kuwa idadi hiyo huenda ikawa mara tano zaidi.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef