1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yadai itaandaa kwa wakati Kombe la dunia 2010

Ramadhan Ali22 Septemba 2006

Ikijibu wasi wasi wa Beckenbauer na wa rais wa FIFA Sepp Blatter, Afrika Kusini imesema maandalio ya Kombe la dunia 2010-la kwanza barani Afrika yatakamilika kwa wakati.

https://p.dw.com/p/CHd9

Bundesliga intrudi uwanjani jumamosi hii huku timu tofauti kabisa ikishika usukani wa ngazi ya Ligi:Hertha Berlin,ghafula imeparamia kilele cha Bundesliga ikiwa mara ya kwanza tangu 2000.Hivi sasa inatetea ngazi hiyo isiwaponyoke katika mpambano na Mainz.

Timu hii kutoka mji mkuu wa Ujerumani inabidi lakini kucheza bila ya stadi wao wa giungo,mturuki Yildiray Bastruk na mbrazil Gilberto.Hatahivyo, berlin imeingia uwanjani na stadi wa Brazil Christian Gimenezo aliekwishatia mabao 4 katika mechi 3 zilizopita.

Mabingwa Bayern Munich wanachuana wakati huu na Alemanna Aachen,timu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu.Munich wana pointi 7 –pointi moja kasoro kuliko Berlin.Mwishoni mwa wiki iliopita,Munich ilizabwa mabao 2:1 na chipukizi Armenia Bielefeld.

Changamoto ya kusisimua zaidi ni kati ya majirani 2 wa kaskazini-Hamburg dhidi ya Bremen.

Katika la Liga, Ligi ya Spain, mabingwa FC Barcelona wanakabiliwa na mtihani wao wa kwanza mgumu msimu huu kesho wakiwa na miadi na Valencia.

-Ama katika Premier League, ligi ya Uingereza, Chelsea-mabingwa wana miadi leo na Fulham.Endapo Chelsea ikitambajumamosi hii,huenda ikarudi kileleni mwishoni mwa wiki hii.Fulham azma yao zaidi itakua kufuta madhambi waliofanya jumatano iliopita walipotolewa nje ya kombe la Ligi na Wycombe .

Katika changamoto za Ligi ya Ufaransa, Olympique Lyon inayoshika usukani na wenzao Olympique Marseille wanaendelea kunyan’ganyia uongozi .Marseille ina pointi 16 na mwanya wa mabao 10 lakini wapo bega kwa bega na Lyon.Lyon wanaumana na Lille.

Brazil chini ya kocha mpya Dunga, imepanga mapambano 2 zaidi ya kirafiki-moja dhidi ya Ecuador hapo oktoba 7 na jengine siku 3 baadae dhidi ya Kuweit.Katika mapambano yote 2, Ronaldo ameachwa kando.

Dunga aliechukua nafasi ya kocha Carlos Alberto Parreira,amewachagua wachezaji 4 wapya wasiowahi bado kuvaa jazi ya Brazil.Wao ni mlinzi wa klabu ya Se villa Daniel Alves na mwenzake Adriano,mchezaji wa kiungo wa klabu ya Gremio Lucas na kipa wa Fc Porto ,Helton.

Katika dimba la Afrika, kinyan’ganyiro cha kuania Kombe la CAF-shirikisho la dimba la Afrika kimerudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii:

Mjini Kinshasa,St.Eloi Lupopo inakabiliwa na changamoto kali ya kufa-kupona hii ileo ikichuana nyumbani na etoile Sahel ya Tunisia.Lupopo lazima ishinde jumamosi au sivyo, itaaga mashindano.

Etoile haitakua ni mteremko kwa Lupopo ,kwani wakongomani watakumbuka duru iliopita jinsi Etoile ilivyoirarua St.Eloi Lupopo mjini Sousse,ilipoizaba mabao 3 mnamo muda wa dakika 5.

Etoile ina pointi 9,Esperante pia ya Tunisia ina pointi 6 wakati St.Eloi Lupopo ina 3.Ushindi leo utaiokoa St.Eloi Lupopo na kuzusha shangwe na shamra shamra mjini Lumbubashi,km 200 kutoka Kinshasa.

Afrika Kusini itaandaa Kombe la kwanza la dunia barani Afrika 2010,lakini jukumu hilo limeanza kutiliwa shaka iwapo itaweza kweli kulibeba:

Danny Jordan ni mwenyekiti wa kamati ya maandalio ya kombe hilo,lakini mwenzake wa Ujerumani-Franz Beckenbauer,ndie miongoni mwa wale walioelezea shaka-shaka iwapo kweli Afrika Kusini itakamilisha matayarisho kwa wakati.

Rais wa FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,Sepp Blatter alifichua wiki iliopita kwamba ana azma ya kuzuru Afrika Kusini hivi karibuni, ili kuiamsha kamati hiyo ya maandalio kuharakisha mambo.

Danny Jordan alikanusha tuhuma za Beckenbauer,akidai Beckenbauer, haelewi mambo hasa yanavyokwenda na hakuna haja ya kuzusha wasi wasi.

Hatahivyo, Jomo Sono, maarufu katika dimba la Afrika Kusini na aliecheza kabumbu pamoja na Beckenbauer na Pele katika klabu ya Cosmos,New York, ameonya kwamba timu ya maandalio ya kombe la dunia 2010 iyazingatie vilivyo maoni alioeleza Beckenbauer.

“Tatizo letu sisi waafrika, ni kuwa hatupendi kukosolewa.”

Jomo Sono akaongeza kusema kwamba yeye hajui ni kitu gani kilichopelekea Beckenbauer kuzungumza hivyo, lakini yafaa aulizwe ,lakini aliyosema yazingatiwe barabara.

Danny Jordan,mwenyekiti wa Kamati ya maandalio ana yakini kuwa Africa Kusini itakamilisha matayarisho kwa wakati.hatahivyo, maafisa wakuu wa m,anicipaa katika miji 9 ambako kombe la dunia litachezwa, waliituhumu serikali ya Afrika Kusini na wabunge mwezi uliopita kukwamisha matayarisho yao ya Kombe la dunia.

Katika medani ya riadha:bingwa wa rekodi ya dunia ya mita 100, mjamica Asafa Powell ameahidi kuvunja rekodi yake ya dunia ya mita 100 mwishoni mwa wiki hii huko Yokohama,Japan.

Powell, mwenye umri wa miaka 23 kutoka Jamaica, amekimbia mbio 12 za masafa ya mita 100 kwa muda wa chini ya sek.10 msimu huu.Aliweza mara 2 kusawazisha rekodi yake ya dunia alioiweka mara ya kwanza mjini Athens, Ugiriki Juni,mwaka jana.Kwa rekodi mpya, Powell amewaambia waandazi huko Japan kuwa, angehitaji hali nzuri ya hewa na upepo usio mkali sana .Changamoto kali atapewa na patrick Johnson wa australia aliekimbia muda wa sek.9.93.