Amani inahitaji wanawake
27 Aprili 2006Kulingana na utafiti wa masuala ya kivita, nusu ya vita vilivyomalizika kwa kufikia makubaliano ya amani, vitalipuka katika miaka mitano baada ya vita hivo kumalizika. Kwa Bibi Ruth Ojiambo Ochieng, sababu ya maendeleo haya ni wazi.
Bibi Ojiambo ni mkurungezi wa shirika la kimataifa la wanawake Isis-WICCE, lenye makao yake makuu nchini Uganda. Anaeleza: “Ukiangalia jinsi wanawake kwenye vyeo vya juu au chini wanavyotambua suala la kuimarisha amani, wanajaribu kubadilisha jamii ili kuondoa athari za vita. Lakini ukisikiliza jinsi wanaume wanavyozungumzia mambo ya amani, hasa ni kuhusu kuacha silaha na kujadili kuhusu masuala ya madaraka na mamlaka. Sisi kama wanawake tunaona aina hii ya amani haiwezi kudumu.”
Na hiyo ndiyo sababu kwa nini makubaliano mengi ya amani, hasa yale yaliyofikiwa barani Afrika, hayakufanikiwa, anasema Bibi Ojiambo, kwani hayazingatia hisia za watu wala hayahusu mahitaji ya wale walionusurika na vita. Katika sehemu ya Kaskazini ya nchi yake Uganda ambapo vita vya kundi la waasi wa LRA dhidi ya serikali ya Uganda vinaendelea, wanawake wanatoa mfano mzuri wa kuunda amani, hata ikiwa vita vinaendelea.
Bibi Ojiambo: “Amani siyo kunyamazisha silaha. Wanawake hawa wanahifadhi kile kiasi kidogo cha amani kilichopo. Wameunda kamati za amani na wameanzisha mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuwasaidia wasichana wanaorudi baada ya kutekwa nyara na waasi wakibeba mimba. Wasichana hawa wanasaidiwa pia kuanza maisha yao upya kwa kufundishwa kazi fulani. Kwa hivyo wanawake huko Kaskazini wamejenga mfumo katika kila daraja, lakini kitu wanachokikosa ni kutambuliwa na kusaidiwa katika kazi zao.”
Juu ya hayo, wanawake pia wanaweza kusaidia kuleta amani hata ikiwa wanawake si wapiganaji. Ruth Ojiambo anatoa mfano kutoka eneo la Kaskazini-Magharibi mwa Uganda ambapo kundi la akinamama lilichukua jukumu la kuwaomba wake wa waasi wa vita wazungumze na waume wao warudi makwao.
Bibi Ojiambo amesema: “Wanawake kwa kweli wana nguvu ndani yao, kwani walipozungumza na waume, kaka au wapenzi wao, wengi wao wamerudi. Na ndiyo njia wanawake wamewaunganisha wapiganaji hao na serikali. Hivyo waasi na serikali wameanza kuzungumza. Wakati ninapoongea hapa, wako nyumbani.”