Ban atangaza dola bilioni 40, kuimarisha afya ya wanawake.
22 Septemba 2010Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema, wanatambua nini kinachoweza kusaidia ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto na kwamba wanafahamu kuwa wanawake na watoto ndio msingi wa malengo ya maendeleo ya milenia.
Ban Ki Moon amekadiria kwamba mkakati wa dunia kwa afya ya wanawake na watoto utaokoa maisha ya watu milioni 16 ifikapo mwaka 2015.
Serikali mbalimbali, wahisani na mashirika binafsi yameahidi kutoa fedha taslimu, kukamilisha mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa juu ya malengo ya maendeleo ya milenia ambao umelenga kuangamiza umasikini, kampeni ambayo iliathiriwa vibaya na msukosuko wa fedha kimataifa.
Wakfu wa watu tajiri kabisa duniani, tajiri wa Mexico Carlos Slim na bilionea Bill Gates mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft ni miongoni mwa waliochangia.
Akisisitizia hilo Waziri Mkuu wa Norway Jens Stoltenberg, ambaye nchi yake ni moja ya wafadhili wakubwa duniani, amesema haijawahi kutokea kwa watu wengi kukusanyika pamoja kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanawake na watoto.
Shirika la Umoja wa mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, Shirika la Afya Duniani WHO na Benki ya Dunia ni miongoni mwa mashirika ya kimataifa yatakayosaidia kuhamasisha kuunga mkono kampeni hiyo ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa.
Akizungumzia kuhusiana na suala la afya ya wanawake, Mkurugenzi mtendaji kutoka katiika shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu -UNFPA- Thoraya Obaid amesema maendeleo katika afya na haki za wanawake ni moja ya masuala muhimu ya kijamii kwa wakati huu.
Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema kuwekeza katika afya ya wanawake na watoto ni masuala yanayostahili kuwa katika ajenda ya juu ya maendeleo.
Kupunguza vifo visivyo vya lazima wakati wa ujauzito na wakati wa uzazi na ukomeshaji vifo vya watoto waliochini ya umri wa miaka mitano ni malengo yanayopiga hatua taratibu katika malengo nane muhimu ya maendeleo yaliyolengwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inasema kwamba vifo vya zaidi ya watoto milioni 15 walio chini ya umri wa miaka mitano vinaweza vikaepukwa kati ya mwaka 2011 na 2015 kupitia hatua mbalimbali.
Taarifa hiyo imeongezea kusema kuwa hatua hizo pia zitasaidia kuzuia vifo vya wanawake 740,000 kutokana na matatizo yanayotokea wakati wa kujifungua na ujauzito. Na kukadiria kuwa watoto milioni 120 watalindwa kutokana na nimonia.
Takriban viongozi na wakuu wa serikali kutoka katika nchi 140 wanahudhuria mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Mataifa, utakaofungwa rasmi na Rais Barack Obama wa Marekani.
Mkutano huo wa siku tatu wa Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuongezwa nguvu zaidi katika malengo manane ya maendeleo yaliyofikiwa katika mkutano wa milenia wa mwaka 2000, ambayo lengo ni kuwa yamefikiwa hadi ifikapo mwaka 2015.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri:Abdul-Rahman