Chad yafanya uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa
29 Desemba 2024Uchaguzi huo umetajwa na serikali kama hatua ya mwisho ya mpito wa kisiasa, baada ya miaka mitatu ya utawala wa kijeshi.
Hata hivyo upinzani umeususia uchaguzi huo ukipinga kile unachokiita ‘mfumo uliojengwa kwenye misingi ya uongo na wizi wa kura'.
Soma pia: Kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa kunawatia wasiwasi Wachad
Kupitia ukurasa wa Facebook, upinzani umewataka wafuasi wao kutojitokeza ukisema matokeo ya uchaguzi huo tayari yapo kwenye makompyuta hata kabla ya kura kupigwa.
Hatua ya upinzani kususia uchaguzi huo imewaacha wagombea wanaoegemea upande wa Rais Mahamat Idriss Itno bila ushindani.
Jenerali Mahamat Idriss Itno, aliwekwa madarakani na jeshi mnamo mwaka 2021 na kisha kushinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Mei mwaka jana ambao wagombea wa upinzani waliukosoa kuwa ulikumbwa na udanganyifu.