1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Idadi ya vifo yakaribia milioni 1 ulimwenguni

Deo Kaji Makomba
21 Septemba 2020

Marekani bado ni taifa lililoathirika pakubwa zaidi kwa maambukizi ya virusi vya corona duniani, wakati kukiripotiwa vifo vinavyokaribia 200,000, huku wimbi la pili la kufungwa kwa shughuli nalo pia likiinyemelea Ulaya.

https://p.dw.com/p/3inKS
USA I Emmy Awards - Preisverleihung 2020
Picha: Invision for the Television Academy/AP/picture-alliance

Lebanon imeorodhesha visa 1,006 vya ugonjwa wa Covid 19 katika saa 24 zilizopita, hii ikiwa ni kulingana na serikali jana Jumapili.   

Waziri wa afya wa Lebanon Hamad Hassan amependekeza wiki mbili za kusimamishwa kabisa kwa shughuli nchini humo ili kudhibiti maambukizi ya kila siku ya virusi vya corona, lakini mamlaka zitakabiliwa na ugumu wa kuanzisha tena hatua kama hiyo katikati ya anguko kubwa la uchumi.

Visa vipya vilivyosajiliwa na wizara ya afya vinafanya jumla ya visa vilivyothibitishwa nchini Lebanon kufikia 29,303 wakati idadi ya vifo ikifikia 297 tangu kuliporipotiwa kisa cha kwanza mwishoni mwa Februari. Ilikuwa ni siku ya tatu mfululizo ya rekodi ya juu kabisa ya maambukizi tangu kuripotiwa kisa cha kwanza mwishoni mwa Februari.

Kuongezeka kwa visa vya maambukizi kulianza baada ya kulegezwa kwa vizuizi vya kutotoka nje na kufunguliwa tena kwa uwanja pekee wa ndege wa kimataifa mapema Julai. Visa viliongezeka zaidi baada ya mlipuko mkubwa uliotokea Agosti 4 katika bandari ya Beirut uliouwa watu193, kujeruhi watu wasiopungua 6,500 na kuharibu sehemu kubwa ya jiji.

Libanon Feuer Brand Beirut
Mlipuko mkubwa uliotokea Lebanon ulisababisha madhara makubwa ambayo ni pamoja na majeruhi na athari za kiuchumi.Picha: Reuters/I. Abdallah

Mlipuko huo pia ulisababisha hospitali za Beirut kuelemewa, lakini pia uliharibu vibaya hospitali mbili zilizokuwa na jukumu kubwa la kuwatibu waathirika wa virusi vya corona.

Nchini Urusi, kumeripotiwa visa vipya 6,196 vya virusi vya corona ambavyo ni vingi zaidi kuwahi kuripotiwa katika kipindi cha masaa 24 tangu Julai 18 na idadi sasa kufikia 1,109,595, hivyo kuwa taifa la nne kwa idadi kubwa ya maambukizi ulimwenguni. Mamlaka pia iliripoti vifo 71 kwa kipindi cha saa 24 zilizopita na kupelekea idadi rasmi ya vifo kufikia 19,489.

Na huko Marekani idadi ya waliofariki kutokana na virusi hivyo ilikuwa inakaribia 200,000 hadi Jumatatu hii. Takriban watu 800 wanakufa nchini Marekani kila wiki kutokana na virusi vya corona, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za shirika la habari la Reuters. Hata hivyo idadi hiyo imeshuka kutoka idadi ya juu kabisa ya kila siku ya 2,806 iliyorekodiwa Aprili 15 mwaka huu.

Mapema mwezi huu, rais Donald Trump alitetea namna anavyoshughulikia tatizo hilo. Alikiri kuliwekea kulipuuza janga hilo huko nyuma wa sababu hakutaka kuwatisha watu.

Zikiwa zimebaki wiki sita kabla ya uchaguzi, Trump yuko nyuma ya mpinzani wake Joe Biden wa chama cha Democratic kitaifa katika kila kura kuu ya maoni huku wakichuana katika majimbo yenye ushawishi mkubwa wa kuamua matokeo.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba/dw.com