1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump na ukuta wa Mexico Magazetini

Oumilkheir Hamidou
20 Februari 2019

:Azma ya rais Donald Trump ya kujenga ukuta, umri mrefu sio sababu ya kutopigania kiti cha rais nchini Marekani na mjadala kuhusu kurejeshwa nyumbani wanamgambo wa itikadi kali ni miongonim mwa mada magazetini .

https://p.dw.com/p/3DiKU
Florida Trump Rede zu Venezuela Krise
Picha: Reuters/K. Lamarque

:

Tunaanzia Marekani ambako rais Donald Trump anakabiliwa na kishindo kikubwa kutoka tangu wabunge wa chama cha Democrat mpaka kufikia baadhi ya magavana wa majimbo ya nchi hiyo. Chanzo ni azma yake ya kutaka kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico . Gazeti la "Schwäbische Zeitung" linaandika: "Upinzani dhidi ya Trump unazidi makali. Magavana 16 wa majimbo wamesimama kidete  na kutuma mashitaka ya pamoja kupinga sheria ya hali ya hatari aliyoitangaza ili apate njia ya kujenga ukuta. Wanasiasa wa Ujerumani wanatambua tafsiri ya kanuni zinazofafanua madaraka ya kiongozi wa serikali. Kifungu nambari 65 cha sheria msingi kinaondowa uwezekano wa kukiukwa jukumu la bunge, kama alivyofanya Trump hivi karibuni. Mtindo wake wa kupitisha maamuzi ya upande mmoja umezusha wasi wasi mkubwa katika sehemu iliyosalia ya dunia.

Ujerumani inasumbuliwa zaidi na mtindo huo. Trump amewahuzunisha mno washirika ndani ya jumuia ya kujihami ya NATO. Kwa mtazamo wa muda mrefu hatoweza Trump kuendelea daima kukiuka muongozo wa sheria nchini mwake. Ujerumani na mataifa rafiki wanakabiliwa na jukumu la kupunguza hasara hadi mapambazuko yatakapotokea. Na maandalizi ya enzi za baada ya Trump hayatokawia."

Kinyang'anyiro cha kuania kiti cha rais wa Marekani kimeshaanza

Miaka miwili kabla ya mhula wa rais wa Marekani Donald Trump kumalizika, wapinzani wake kutoka chama cha Democratic wameshaanza kuuvalia njuga wadhifa huo. Mbali na wanasiasa kadhaa  mashuhuri wa kike, Bernie Sanders aliyeshindana na Hillary Clinton katika kinyang'anyiro cha kuania tikiti ya chama cha Democratic kwa uchaguzi wa mwaka 2016, ameamua kujibwaga upya mashindanoni, uchaguzi utakapoitishwa mwaka 2021. Gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger linaandika: "Tunaweza kushuku kama mzungu wa miaka 77 anafaa kukabidhiwa bendera ya chama kinachowavutia zaidi wanawake na wapiga kura wenye asili ya kiafrika.

 Zaidi ya hayo mwanasiasa huyo anaezusha mabishano hana haiba ya kuweza kuiunganisha nchi hiyo iliyogawanyika. Na hiyo ndio changamoto kubwa zaidi inayowakabili wademokrats: Wanabidi wampate mgombea atakaekuwa na kipaji cha kuwazinduwa walioko mashinani. Mgombea huyo, awe mwaname au mwanamke hatakiwi kuwa kitisho kwa wapiga kura wa mrengo wa wastani."

Vipi magaidi wa IS warejeshwe nyumbani?

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha Ujerumani ambako mjadala umepamba moto kuhusu namna ya kuwarejesha nyumbani magaidi wa kile kinachoitwa "Dola la Kiislam-IS".Gazeti la "Donaukurier" linaandika: "Donald Trump anachekelea jinsi alivyofanikiwa kuwatia mashakani viongozi wa ulaya. Ilitosha kutuma risala kupitia mtandao wa twitter tu kutishia wanamgambo wa kigaidi wa IS wataachiwa huru. Wale magaidi wa IS ambao hawashikiliwa na Marekani lakini. Wakati huo huo amewatahadharisha washirika wake watawajibishwa kisheria-akijisahau mwenyewe kuwa ni rais wa nchi ambayo kwa miaka sasa inasimamia kambi ya Guantanamo bila ya kuheshimu sheria wala misingi ya haki za binaadam."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Sekione Kitojo