Elon Musk amtusi Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
1 Januari 2025Matamshi ya Musk yalimlenga Steinmeier akizungumza dhidi ya ushawishi wa nje katika hotuba yake kuhusu kuvunjwa kwa bunge la Ujerumani - Bundestag. Ujumbe wake kwenye X ulikuwa jibu kwa ukosoaji wa Steinmeier, ambaye ni mkuu wa nchi, uliofanywa na mshawishi wa mitandaoni Naomi Seibt anayegemea chama cha mrengo mkali cha Mdadala kwa Ujerumani - AfD.
Musk amemuita Steinmeier kuwa mbabe anayepinga demokrasia. Ofisi ya Steinmeier imesema kuwa imeuona ujumbe huo lakini haitatoa kauli yoyote.
Baada ya kuvunjika kwa serikali ya muungano ya Ujerumani ya pande tatu mwezi Novemba, Musk alimuita Kansela Olaf Scholz kuwa mpumbavu kwa Kijerumani.
Katika ujumbe wa awali, Musk alitabiri kuwa Scholz atashindwa kwenye uchaguzi ujao wa Ujerumani Februari mwakani. Akaunti ya Musk ya X, mtandao anaoumiliki, ina zaidi ya wafuasi milioni 200. Naibu Kansela wa Ujerumani Robert Habeck pia alimshutumu Musk kwa majaribio yake ya kushawishi uchaguzi wa Ujerumani.