England yaibwaga Scotland kombe la dunia wanawake
10 Juni 2019Mabingwa wa zamani Japan watakuwa na matumaini ya kukimbizana na mahasimu wao katika kundi hilo England ambao walianza kwa kushinda jana Jumapili wakati kikosi hicho maarufu kama Nadeshiko kikifungua kampeni yake katika kombe la dunia dhidi ya Argentina leo Jumatatu.
England waliwashinda mahasimu wao wakubwa Scotland mjini Nice jana Jumapili, licha ya kikosi hicho cha kocha Phil Neville kulazimika kulinda kwa njia zote ushindi wao wa mabao 2-1 kwa muda mrefu wa mchezo huo.Engalnd ambayo ni moja kati ya timu zinazopigiwa upatu kutoroka na taji hilo, ilinyakua pointi zote tatu katika kundi D katika mchezo uliopigwa kusini mwa Ufaransa, lakini Scotland ilibambana katika kipindi cha pili katika mchezo wao wa kwanza kushiriki katika kombe la dunia na Claire Emslie alipata bao moja.
Kocha wa England Phil Neville amesema baada ya mchezo huo kwamba timu yake haiwezi kumudu kuthubutu kupoteza kasi ya mchezo wake , na inapaswa kucheza kwa ukakamavu ule ule na kumiliki mpira iwapo inataka kusonga mbele katika kombe la dunia la wanawake.
Ante Milicic ana siku nne kuweza kuipa uhai timu yake ya wanawake wa Australia katika kampeni ya kombe la dunia baada ya kushindwa na Italia na hakuna kitakachopuuzwa kabla ya kukabiliana na Brazil mjini Montpellier siku ya Alhamis.
Australia kwa jina la utani Matildas, walishangazwa kwa bao la dakika za mwisho la barbara Bonansea kwa kichwa jana, na kuipa Italia, Squadra Azzurre kwa mabao 2-1 katika kundi C.
Astralia itapambana na Brazil , ambayo ilifungua kampeni yake kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Jamaica na kujihakikishia nafasi nzuri kuelekea katika timu 16 zitakazoingia katika duru ya mtoano.