England yatinga robo fainali licha ya utata wa VAR
24 Juni 2019Cameroon walionekana kukasirishwa kabisa mara mbili na maamuzi ya refa yaliyotokana na mfumo wa VAR ambayo hayakuwaendea sawa huku mwamuzi akionekana kushindwa kuidhibiti hali.
Baada ya bao la pili la England la Ellen White mwishoni mwa kipindi cha kwanza kufutwa awali kwa sababu ya kuotea, na kisha kukubaliwa tena kupitia VAR, wachezaji kadhaa wa Cameroon walimfokea refarii.
Cameroon kisha wakadhani wamerejesha bao moja, kabla ya kufutwa na VAR kwa sababu lilikuwa la kuotea hali iliyozusha rabsha zaidi uwanjani. Mechi ilisitishwa kwa muda huku wachezaji wacameroon wakikataa kucheza lakini ikabidi kocha wao awatulize ili mchezo uendelee.
Mechi hiyo kisha ikageuka kuwa mbovu huku matukio ya kucheza ngware yakishuhudiwa na pamoja na tuhuma za kuwatemea mate wenzao zikikithiri. Kisha Alexandra Takounda akampiga kiasi Steph Hougton wa England na tena baada ya kuangalia VAR, akapewa kadi ya njano, na ilihali ingekuwa nyekundu. Kocha wa England Phil Neville alijawa na ghadhabu akisema alichokiona sio kandanda.
England watakutana na Norway katika robo fainali baada ya timu hiyo ya Scandinavia kuilaza Australia kupitia penalti Jumamosi. Aidha Ujerumani ilitinga robo fainali baada ya kuifunga Nigeria 3 – 0.
Wenyeji Ufaransa walijikatia tiketi ya robo fainali baada ya kuwafunga Brazil 2 – 1 katika muda wa ziada. Hii leo timu mbili zaidi zitajikatia tiketi ya hatua ya robo fainali. Uhispania itacheza na mabingwa watetezi Marekani wakati Sweden ikiangushana na Canada. Kesho Jumanne, Italia itacheza na China huku Uholanzi ikipinga na Japan.
Mwisho wa michezo kwa sasa, kwa mengi zaidi tembelea ukurasa wetu wa michezo, fungua dw.com/Kiswahili. Mimi ni Bruce Amani, kwaheri kwa sasa