Erdogan: Ethiopia na Somalia wameafikiana kumaliza mzozo
12 Desemba 2024Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo yaliyofanyika jana Jumatano, kwa saa kadhaa mjini Ankara.
Akiyasifu makubaliano hayo ya kihistoria katika mkutano wa pamoja na waandishi habari, Erdogan amesema ana matumaini kwamba mpango huo utakuwa hatua ya kwanza kuelekea mwanzo mpya unaozingatia amani na ushirikiano kati ya Somalia na Ethiopia.
''Pamoja na michango ya nchi zote mbili, tumeandaa tamko la pamoja ambalo tumekubaliana leo. Tamko hili la pamoja linarekodi kanuni ambazo nchi hizi mbili rafiki, zilizo muhimu sana kwetu katika kuziangazia siku zijazo, na sio yaliyopita. Na haya yatafanywa kuanzia sasa.'' amesema kiongozi huyo.
Erdogan amewashukuru Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kwa kufikia makubaliano hayo ya kihistoria. Amesema Ethiopia na Somalia zina nia ya kushirikiana pamoja.