1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali za kombe la dunia kwa wanawake kuanza Jumapili

24 Juni 2011

Fainali za FIFA za kombe la dunia kwa wanawake zinaanza rasmi Jumapili nchini Ujerumani, wakati mabingwa watetezi Ujerumani itakapofungua dimba na Canada katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/11iz2
Timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani itakayofungua dimba Jumapili kwa kupambana na Canada.Picha: picture alliance/dpa

Fainali za kombe la dunia la shirikisho la kandanda duniani FIFA kwa wanawake zinaanza rasmi kesho Jumapili nchini Ujerumani wakati mabingwa watetezi Ujerumani watakapoanzisha tena juhudi zao za kulinyakua tena kombe hilo kwa mara ya tatu. Ujerumani inafungua dimba na Canada katika mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Olimpiki wa mjini Berlin. Na huko mjini Dar Es Salaam leo jioni vumbi litatimka wakati mabingwa wa soka Tanzania bara Dar Young African watakapotiana kifuani na El-Mereikh ya Sudan katika uwanja wa taifa katika pambano la ufunguzi la kombe la klabu bingwa la Kagame kwa vilabu vya mataifa ya Afrika mashariki na kati.

Mabingwa watetezi Ujerumani wanazindua kampeni yao ya kuwania kulitwaa tena kombe la dunia kwa kandanda la wanawake katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin , ambapo rais wa Ujerumani Christian Wulff na kansela Angela Merkel watakuwa wageni rasmi katika pambano hilo la ufunguzi. Timu mbili kutoka bara la Afrika zinashiriki fainali hizo. Timu hizo zinazowakilisha bara la Afrika ni Nigeria na Guinea ya ikweta.

Mabingwa wa kombe hilo la dunia kwa wanawake Ujerumani kwa mwaka 2003 na 2007 wanategemea kuungwa mkono kwa nguvu na mashabiki wa nyumbani huku watayarishaji wakiwa tayari wameuza asilimia 80 ya tiketi zote 900,000 kwa ajili ya mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia tarehe 26 Juni hadi Julai 17.

Tuna ndoto na hii ni kushinda kombe hili hapa nyumbani. Tutafanya kila linalowezekana kutimiza ndoto hiyo, amesema kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Silvia Neid, ambaye amerefusha mkataba wake hadi mwaka 2016 siku chache tu zilizopita.

Deutschland - Norwegen
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Silvia, ana matumaini ya kulinyakua kombe la dunia mara ya tatu.Picha: picture alliance / dpa

Katika wiki za hivi karibuni , wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani pamoja na kocha wao wamejikuta nyuso zao zikiwa kila mahali katika kurasa za mbele za vyombo vya habari. Maeneo ya kuangalia kandanda ya wazi yamekwisha tayarishwa katika miji ili kuweza kuwapa nafasi watu wengi kuangalia michuano hiyo.

Alipoulizwa kuhusu ni umbali gani Ujerumani inaweza kwenda katika mashindano haya, rais wa Ujerumani Christian Wulff alijibu, "mabingwa wa dunia". Nataraji kuona michezo ya haki na yenye msisimko mkubwa na natumai kuwa timu yetu itafikia fainali na kushinda, amesema rais huyo wa Ujerumani Christian Wulff.

Lakini balozi maalum wa kutangaza mashindano haya wa Ujerumani Sharry Reeves hata hivyo ana mtazamo tofauti kuhusu fainali za mwaka huu, ambazo ni za sita kufanyika kwa wanawake.

"Haitakuwa kama kila mtu anavyotarajia, kwasababu kila mtu anafikiria kuwa Ujerumani , ni timu nzuri sana na tunataka kushinda na timu nyingine haziwezi kucheza kabisa. Sifikirii hivyo, nafikiri kutakuwa na mshangao mkubwa na kila timu itaonyesha ustadi wao pia kama Ujerumani. Na la pili tutawaona wachezaji nyota chipukizi katika mashindano haya kama Alexandra Popp, ambaye ni mchezaji kijana sana. Alikuwa mwaka jana mchezaji bora katika mashindano ya kombe la dunia la vijana chini ya miaka 20, pamoja na golikipa bora, kwa hiyo kutakuwa na mshangao mkubwa".

WM Fussball U20 Frauenfussball
Mchezaji nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani ya wanawake Alexandra Popp.Picha: picture alliance/dpa

Timu ya taifa ya Marekani ambayo inawekwa katika nafasi ya miongoni mwa vigogo wa soka la wanawake, ikiwa imelitwaa kombe hilo mara mbili hapo nyuma pamoja na kuwa mabingwa wa sasa wa Olimpiki , itatoa changamoto kubwa katika fainali hizi zinazojumuisha timu 16. Brazil ikiongozwa na mchezaji bora wa mwaka mara tano duniani ,Marta , inatafuta ufunguo wa kulinyakua kombe hili kwa mara ya kwanza. Iwapo tutakuwa katika kiwango chetu cha juu hakuna timu duniani inayoweza kutubwaga, amesema mshambuliaji wa Marekani Abby Wambach.

Fußballerin Marta Brasilien
Mchezaji wa kiungo wa Brazil Marta, ambaye ni mchezaji bora wa mwaka kwa muda wa miaka mitano sasa.Picha: dapd

Wakati nyasi zinatayarishwa kwa ajili ya mpambano huo wa fainali za kombe la dunia hapo kesho huko mjini Berlin , huko Dar Es Salaam jioni ya leo nyasi ziliaanza kuwaka moto, wakati mabingwa wa soka Tanzania Bara Dar Young Africans, "Yanga" wanakana koo katika uwanja wa taifa mjini Dar Es Salaam na mabingwa wa Sudan El-Mereikh katika mashindano ya kuwania kombe la Kagame la vilabu katika Afrika mashariki na kati.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman