1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ngumu inayowakumba wakimbizi wanawake

Mohammed AbdulRahman16 Machi 2006

Ripoti ya tume ya wakimbizi wanawake na watoto yenye makao yake makuu mjini New York, ni kwamba takriban watu 35 milioni duniani wanaishi katika hali ya kutawanyika baada ya kuyahama makaazi yao ndani katika nchi zao wenyewe au katika mipaka ya kimataifa kwa sababu mbali mbali vikiwemo vita.

https://p.dw.com/p/CHna
Wanawake huko Darfur na mzigo wa kuni vichwani.
Wanawake huko Darfur na mzigo wa kuni vichwani.Picha: AP

Lakini kwa wanawake na wasichana wanaoishi katika hali hiyo, maisha yanazidi kuwa magumu na vitisho vinavyoandama maisha yao ya kila siku vinazidi kuwa vikubwa.

Wakilazimika kuyahama makaazi yao kwa sababu ya vita, na kuandamwa na majanga ya kimaumbile, jumla ya watu 35 milioni kote duniani wanasemekana wanaishi wametawanyika ndani katika nchi zao au katika mipaka inayotambuliwa kimataifa. Kila siku mamilioni ya wanawake na wasichana hukusanya kuni kwa ajili ya familia zao katika mazingira ya hatari na kukabiliwa na kitisho cha kubakwa, kutekwa nyara, kuibiwa na hata kuuwawa. Hayo yamesisitizwa katika ripoti ya tume hiyo ya wanawake na Mkurugenzi mtendaji Carolyn Makinson. Akiongeza kwamba wanakua hawana chaguo jengine, kwani ni jambo la kutapia maisha.

Makambi ya wakimbizi na watu waliotawanyika panapaswa kuwa mahala pa usalama, na penye ulinzi na kinga pamoja na kuwa ni pa kuwasaidia wale wenye mahitaji kutokana na yale yaliowasibu. Lakini wakati makaazi, maji, huduma ya afya na chakula ni mahitaji yanayotolewa, ni nadra kwao kupewa mafuta yanayohitajika kupigia chakula. Kutokana na hayo wanalazimika kutafuta njia nyengine na katika hatua hiyo hukabiliwa na hatari zilizotajwa.

Mafuta ya kupikia ni muhimu takriban kwa kila mtu duniani, kwani ndiyo njia ya kupata mlo. Wanawake na wasichana wengi kwa hivyo huanza kazi ya kutafuta cha kupikia tangu mapema na mara nyingi huwa ni kusafiri masafa kusaka kuni. Mfano mmoja : Katika kambi ya waliotawanyika ya Abu Shaouk katika jimbo la Sudan la Darfur, wanawake na wasichana huamka kuanza kutafuta kuni saa 9 za usiku. Hufanya hivyo wakiwa katika makundi madogo madogo, Kila moja likielekea njia yake tafauti katika maeneo yaliozungukwa na jangwa na kujaribu kurudia kambini wakati muwafaka kutayarisha chai ya asubuhi.

Wolfgang Trautwein, Naibu wa muakilishi wa Ujerumani katika umoja wa mataifa alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuwakinga wanawake na wasichana wanaojikuta katika mazingira hayo, huku akisisitiza lakini kwamba ni kwa kuyaelewa tu maisha yao ya kila siku, ndipo hatua madhubuti zinaweza kupitishwa na kuwakinga dhidi ya matumizi ya nguvu yenye misingi ya kijinsia, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya vita. Wito kama huo ulitolewa pia na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la idadi ya wakaazi la umoja wa mataifa Thoraya Ahmed Obaid.

Miongoni mwa yaliopendekezwa katika ripoti ya tume ya wanawake kwa ajili ya wanawake na wasichana waliotawanyika na kuishi kama wakimbizi ndani katika nchi zao na nje ya mipaka ya nchi hizo, ni pamoja na kuanzisha doria za kuwasindikiza kusaka mahitaji yao kama kuni na kadhalika.

Ripoti hiyo imekuja katika wakati ambao umoja wa mataifa umezitaka taasisi na serikali zote duniani kuhakikisha usawa wa kushiriki wanawake katika utoaji maamuzi na kuchukua hatua za kuimarisha mchango wao katika maendeleo.