Idadi ya Maseneta Wanawake kuongezwa Burundi
30 Julai 2005Bujumbura:
Mwenyeiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Burundi, Bw. Paul Ngarambe, ametangaza leo kuwa ataongeza Wanawake wengine watatu katika Baraza la Seneti lililochaguliwa jana. Ongezeko hilo litahakikisha kuona kuwa uwakilishi wa akina mama katika Seneti unafikia asili mia 30 kama vile inavyotakiwa na mkataba wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Bw. Ngarambe, amewaambia Wandishi wa Habari kuwa kuna Wanawake 8 miongoni mwa Maseneta wote 34 waliochaguliwa jana wakati ambapo jumla ya Wanawake waliokuwa wanahitajiwa ni 11. Ili kiwango cha asili mia 30 kiweze kufikiwa lazima idadi hiyo iongezwe. Chama kilichokuwa cha waasi wa Kihutu ambao ni wengi FDD kimepata viti 30 kati ya 34. Chama tawala cha Wahutu FRODEBU kimepata viti vitatu na mshirika wa FDD, CNDD kimepata kiti kimoja. Watwa watapewa viti vitatu na waliokuwa Marais wanne wa Burundi ambao ni hai kila mmoja atakuwa na kiti chake katika Baraza la Seneti lenye Wajumbe 41.