1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lawalaumu wakuu wa maandamano kuhusu vurugu

10 Juni 2019

Jeshi la Sudan limewalaumu wakuu wa maandamano kuendeleza vurugu. Jeshi limetuma vikosi vyake maeneo mbalimbali ya nchi kulinda usalama. Mnamo Jumapili watu 4 waliuawa kufuatia mvutano unaoendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/3K7qO
Sudan - Generalleutnant Shamseddine Kabbashi
Sudan - Generalleutnant Shamseddine Kabbashi
Picha: Getty Images/M. El-Shahed

Baraza la kijeshi linalotawala nchini Sudan limelishutumu vuguvugu linaloongoza maandamano nchini humo kwa kuendeleza machafuko, huku mgomo wa kitaifa wa siku mbili ulioitishwa na wakuu wa vuguvugu hilo ukiendelea.

Wakati huo huo watu wanne wameuawa jana wakati maafisa wa usalama walipokuwa wakitawanya maandamano kutokana na uasi wa kiraia ulioanzishwa jana. 

Tofauti na Jumapili, shirika la habari la AFP limeripoti Jumatatu kuwa maduka kadhaa, vituo vya kuuza mafuta na mabasi yameanza kuhudumu, ikiwa ni siku ya pili ya uasi ulioitishwa wa kiraia dhidi ya baraza la kijeshi.

Lakini wakuu wa waandamanaji wamewahimiza Wasudan kuendelea na uasi, ili kulishinikiza jeshi kuachia madaraka.

Hapo jana Jumapili, maandamano yalianza upya huku watu wakichoma moto matairi barabarani na kuweka vizuizi barabarani katika wilaya ya Bahari, kaskazini mwa mji mkuu Khartoum. Masoko na maduka yaliendelea kufungwa sawa na katika miji mingine.

Lakini maafisa wa polisi waliingilia kati haraka kwa kufyatua risasi hewani pamoja na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji na wakaondoa vizuizi vilivyowekwa barabarani.

Wakuu wa waandamanaji wameitisha uasi wa kiraia dhidi ya baraza la mpito la kijeshi
Wakuu wa waandamanaji wameitisha uasi wa kiraia dhidi ya baraza la mpito la kijeshiPicha: Reuters

Baraza la kijeshi la utawala wa mpito limewalaumu waandamanaji kwa kueneza machafuko hayo. Luteni Jenerali Jamaleddine Omar ambaye anatoka katika baraza la kijeshi linaloongoza amesema kwa kuziba barabara na kuweka vizuizi, waandamanaji walifanya uhalifu.

Jenerali Jamaleddine amesema vikosi vinavyoshughulikia masuala ya dharura vimepelekwa katika maeneo mbalimbali nchini kulinda usalama:

"Baraza la kijeshi limeamua kuwapeleka wanajeshi wa kushughulikia hali ya dharura na wale wa kawaida, ili kurejesha hali ya kawaida na kuwalinda watu ambao hawana silaha. Ili wafungue barabara kuwezesha usafiri wa umma na kulinda taasisi mbalimbali pamoja na masoko.”

Kamati ya madakatari wanaohusishwa na maandamano hayo imesema watu wawili waliuawa wakati wa makabiliano mjini Khartoum na wengine wawili waliuawa katika mji wa Omdurman mkabala na mto Nile.

Vifo vya hivi karibuni vya watu wanne vinafuata vile vilivyotokea wiki iliyopita ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa.

Chanzo cha vifo hivyo ni mvutano kati ya waandamanaji na wanajeshi, ambapo waandamanaji wanalitaka baraza la kijeshi kukabidhi madaraka kwa uongozi wa kiraia. Mgogoro huu umejiri baada ya miezi miwili tangu aliyekuwa rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashiri kuondolewa madarakani Aprili 11.

Chama cha wataalam nchini Sudan ambacho kilianzisha maandamanao dhidi ya aliyekuwa rais Omar Bashir mnamo mwezi Disemba, kimesema kampeni dhidi ya wanajeshi itaendelea hadi watawala wa kijeshi watakapoachia madaraka utawala wa kiraia.