1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jimbo la 51 la Marekani? Canada inavojiandaa kumkabili Trump

12 Januari 2025

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuiwekea Canada ushuru wa asilimia 25 na kudokeza hata juu ya uwezekano wa kuziunganisha nchi hizo mbili. Wataalamu wanasema mzozo kati yao utakuwa na athari kubwa.

https://p.dw.com/p/4p51u
Canada Toronto 2023 | Mnara wa CN ukiwa na mandhari ya Jiji
Uchumi wa Canada unaweza kuingia kwenye mdororo iwapo Trump ataweka ushuru wa asilimia 25.Picha: Valerie Macon/AFP/Getty Images

"Ilaumu Canada!" ni wimbo wa mzaha kutoka filamu ya katuni ya mwaka 1999 "South Park: Bigger, Longer & Uncut," ambapo mama mmoja anahamasisha mji mdogo wa Colorado kupinga uharibifu wa maadili kwa vijana. 

Miaka kadhaa baadaye, Rais mteule Trump anaonekana kuwa na msimamo sawa, akiilaumu Canada kwa uhamiaji haramu na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia mpaka wa kaskazini.

Wiki chache baada ya kushinda muhula wa pili, Trump alitishia kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote za Canada, ikiwemo magari na vipuri, mara tu baada ya kuingia ofisini. 

Trump ameongeza kauli zake kali, akitania kwamba Canada inaweza kuunganishwa kama jimbo la 51 la Marekani na hata kumkejeli Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, aliyejiuzulu hivi karibuni, akimwita "Gavana" wa "Jimbo Kuu la Canada." 

Ni mbwembwe za Trump au kitisho cha kweli?

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kauli hizi ni mbwembwe za kawaida za Trump, lakini wanasiasa na wachumi wa Canada wamezitaja kuwa zisizokubalika, kwani Canada haikuwa lengo kuu la Trump wakati wa kampeni zake, tofauti na China, Mexico, BRICS na NATO. 

"Imetokea ghafla sana," alisema Douglas Porter, mchumi mkuu wa Benki ya Montreal (BMO), akimaanisha shambulio la Trump. "Hakukuwa na shinikizo lolote kati ya wafuasi wake dhidi ya Canada … kwa hivyo hili linatia wasiwasi zaidi." 

Soma pia: Trump atangaza ushuru kwa bidhaa za Mexico

Porter alisema sababu za Trump zinaonekana kubadilika anapokaribia kuingia madarakani Januari 20. 

Canada Brampton 2023 | Magari kwenye mstari wa kuunganishwa katika kiwanda cha Stellantis
Kanada ilizalisha zaidi ya magari milioni 1.5 mwaka 2023, mengi yakiwa kwa ajili ya soko la Marekani.Picha: Chris Young/The Canadian Press/ZUMA Press/picture alliance

Trump, licha ya kushiriki na kusaini Mkataba wa Biashara wa Marekani-Mexico-Canada (USMCA) mwaka 2020, sasa anasema majirani wa Washington wameshindwa kutimiza masharti muhimu ya makubaliano hayo, kuanzia udhibiti wa mipaka hadi biashara. Makubaliano hayo yanatarajiwa kufanyiwa mapitio mwaka ujao. 

"Trump anajulikana kwa kubatilisha makubaliano yake mwenyewe ili kupata makubaliano bora zaidi," alisema Tony Stillo, Mkurugenzi wa Uchumi wa Canada katika kampuni ya ushauri ya Oxford Economics. 

Trump asema Canada inapokea ruzuku ya Marekani

Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social wiki iliyopita kuwa nakisi ya biashara ni ruzuku ya Marekani kwa Canada, akisema uchumi wa Marekani ambao ni mkubwa zaidi duniani "hauwezi kuhimili nakisi kubwa za biashara ambazo Canada inategemea kustawi." 

Biashara kati ya Marekani na Canada ni mojawapo ya ushirikiano mkubwa na uliounganishwa zaidi duniani. Katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka 2024, biashara yenye thamani ya dola bilioni 699.4 ilifanyika kati ya nchi hizo mbili.

Canada ni soko kubwa zaidi la bidhaa za Marekani, ikizitangulia Mexico, Ulaya, na China. Bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani ni pamoja na malori, magari, vipuri vya magari, pamoja na mafuta ya kisukuku.

Soma pia: Marekani kuamua Juni juu ya ushuru wa bidhaa za chuma kutoka EU

Marekani pia ni soko kuu la bidhaa za nje za Canada, ambapo zaidi ya robo tatu ya bidhaa na huduma zinazouzwa nje hupelekwa kusini mwa mpaka. Kwa kulinganisha, asilimia 53 ya bidhaa za Ujerumani huuzwa katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.

Canada Calgary 2024 | Uchimbaji mafuta
Licha ya Marekani kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta, nchi hiyo inaagiza mamilioni ya mapipa ya mafuta ghafi kutoka Canada.Picha: Jeff McIntosh/The Canadian Press/AP Photo/picture alliance

Mafuta ghafi yanachukua robo ya bidhaa zinazouzwa na Canada kwenda Marekani, ambapo mnamo Julai 2024, mauzo hayo yalifikia rekodi ya mapipa milioni 4.3 kwa siku, kulingana na Mamlaka ya Taarifa za Nishati ya Marekani (EIA).

Kwa sababu ya uwezo mkubwa wa usindikaji wa mafuta nchini Marekani, nchi hiyo huchakata mafuta ghafi na kuyageuza kuwa petroli, dizeli, na mafuta ya ndege kwa matumizi ya ndani na kuuza nje tena — baadhi yake yakirudi Canada.

Changamoto kwa sekta za mafuta na magari

Danielle Smith, waziri mkuu wa jimbo la Alberta lenye utajiri wa mafuta, alionya kuwa Marekani ingejiathiri yenyewe ikiwa Trump atatekeleza vitisho vyake, akisema kuwa ushuru wowote uliopendekezwa utawaumiza wazalishaji wa mafuta wa Marekani na kuongeza gharama kwa watumiaji. 

Sekta ya magari ya Canada pia imekuwa shabaha ya hasira za Trump, ambaye anasema kuwa uzalishaji umehamia Canada, na kusababisha kufutwa kazi kwa wafanyakazi wa Marekani.

Soma pia: Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vyapamba moto

Hata hivyo, sekta ya magari ya Amerika Kaskazini imeunganishwa kwa kiwango kikubwa, na vipuri na magari huvuka mpaka wa Marekani na Canada mara kadhaa wakati wa uzalishaji.

Ufisadi waongezeka Marekani chini ya utawala wa Trump

Wakuu wa kampuni za magari nchini Canada wameonya kuwa ushuru unaweza kuvuruga minyororo changamano ya usambazaji, hali ambayo itasababisha ongezeko la gharama na ukosefu wa ufanisi, na hivyo kupandisha bei za magari mapya katika nchi zote mbili.

"Iwapo utatoza ushuru wa asilimia 25 kila wakati kipuri cha gari kinapovuka mpaka, gharama zitakuwa kubwa mno," William Huggins, profesa msaidizi katika Shule ya Biashara ya DeGroote ya Chuo Kikuu cha McMaster, aliiambia DW.

Wiki iliyopita, BNN Bloomberg ya Canada imenukuu wachumi wakisema ushuru wa Marekani unaweza kupunguza pato la taifa (GDP) la Canada kwa asilimia 2 hadi 4 na huenda ukasababisha uchumi wa nchi hiyo kuingia katika mdororo.

Canada yaandaa hatua za kisasi

Chama tawala cha Liberal nchini Canada hakitachagua mrithi wa Trudeau hadi Machi 9, lakini watunga sera wa Canada tayari wameandaa orodha ya bidhaa za Marekani zitakazokumbwa na ushuru wa kulipiza ikiwa Trump ataendelea na mpango wake. 

Wachambuzi waliozungumza na DW walisema Canada huenda ikachagua bidhaa nyeti kisiasa na kiuchumi, kama ilivyofanya wakati wa mzozo sawa wa kibiashara na Trump mwaka 2018. 

Soma pia: Maoni: Mshindi ni jumuiya ya Umoja wa Ulaya

Hata hivyo, bado haijulikani wazi Trump anataka nini hasa. Je, vitisho vya ushuru ni mbinu ya mazungumzo kuhusu udhibiti wa mipaka, ushirikiano wa nishati na magari, au mchango wa Canada kwa NATO? 

"Licha ya usumbufu wa muda mfupi kwa uchumi wa nchi zote mbili, viongozi wa Canada huenda wakaangazia mpango wa muda mrefu kwa sababu moja wazi," alisema Huggins, mchumi wa Chuo Kikuu cha McMaster. 

"Miaka 30 kutoka sasa, Donald Trump hatakuwa hai, lakini Canada itakuwepo," alisema Huggins.