Kansela Merkel akutana na baadhi ya viongozi wa Afrika
12 Juni 2017
Kansela Angela Merkel atakutana na viongozi wa Tunisia, Rwanda, Senegal, Côte d'Ivoire Ghana, Mali, Ethiopia, miongoni mwa wengineo . Lengo ni kuimarisha ushirikiano kwaajili ya maendeleo ya kudumu ya mataifa ya Afrika.
Tayari mwezi Marchi mwaka huu, katika mkutano wa mawaziri wa fedha G-20, mawaziri wa fedha wa mataifa makubwa kiuchumi duniani waliwaalika wenzao wa Côte d'Ivoire, Maroco, Rwanda na Tunisia kushirikiana nao katika kubuni ushirikiano uliopewa jina "Compact with Afrika".
Mkutano huu wa siku mbili unaoanza leo mjini Berlin, chini ya mwezi mmoja kabla ya mkutano wa kilele wa G-20 mjini Hamburg umelenga kuimarisha ushirikiano pamoja na yale mataifa ya Afrika yaliyodhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi pamoja na wawekezaji wa kifgeni watakaosaidia kuinua ajira na kubuni nafasi za kazi barani Afrika.
Misaada ya maendeleo inafungamanishwa na masharti
Akizungumzia kuhusu ushirikiano pamoja na mataifa ya Afrika waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller ameshurutisha kutiliwa maanani miongoni mwa mengineyo "mapambano dhidi ya rushwa, kuanzishwa idara maalum ya hesabu na idara ya kodi ya mapato. Waziri Gerd Müller anaendelea kusema: "Mapendekezo hayo tumeyafikisha mbele ya mataifa yote ya Afrika. Lakini tunaanza na mataifa haya kwanza.Tunasema fedha na ushirikiano itawezekana tu ikiwa masharti fulani yatatekelezwa, inamaanisha kwa mfano mapambano dhidi ya rushwa, kuanzishwa idara ya hesabu na idara ya kodi ya mapato.Tunawaambia wanaotaka kuifuata pamoja nasi njia ya kupambana na rushwa, kuleta uwazi na kuheshimu haki za binaadam, jaza ya juhudi hizo itakuwa kubwa kupita kiasi."
Mkakati wa Ujerumani ni wa maana lakini hautoshi linasema shirika la ONE
Uhusiano wa dhati wa kiuchumi pamoja na Afrika ni kipa umbele cha Ujerumani kama mwenyekiti wa kundi mataifa 20 yaliyoendelea na yanaendelea-G-20. Ingawa kansela Angela Merkel na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble kila kwa mara wanatilia mkazo uwezo mkubwa wa kiuchumi wa bara jirani la Afrika lakini katika medani ya biashara hali ni tofauti. Biashara jumla ya Ujerumani kwa Afrika mwaka 2016 imepungua kwa asili mia mbili na kusalia Euro bilioni 46 ikilinganishwa na mwaka mmoja kabla. Shirika lisilomilikiwa na serikali linalofuatilizia mkutano wa G-20, ONE ingawa linasifu mkakati wa serikali ya Ujerumani kuelekea Afrika hata hivyo linahisi mapendekezo yaliyotolewa hayatoshi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/Reuters
Mhariri:Josephat Charo