1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel atangaza rasmi kugombea muhula wa nne

Daniel Gakuba
21 Novemba 2016

 Kansela Angela Merkel amesema atagombea muhula wa nne katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Bi Merkel ametoa tangazo hilo mjini Berlin akisimama mbele ya bango la Chama chake cha Kihafidhina, Christian Democratic Union, CDU.

https://p.dw.com/p/2SzHF
Angela Merkel kandidiert erneut
Kansela Merkel, akitangaza nia ya kugombea muhula wa nnePicha: Getty Images/S. Gallup

Akizungumza mbele ya vyombo vya habari jioni ya jana Jumapili, Bi Merkel ambaye amekuwa katika wadhifa wa ukansela kwa miaka 11 iliyopita, amesema uamuzi wake wa kugombea tena haukuwa na 'thamani ndogo', iwe kwa nchi yake, au kwake binafsi. Amesisitiza sababu ya kugombea tena ina misingi katika kutumia vipaji vyake kuitumikia Ujerumani.

''Nimekiambia chama changu, CDU kwamba niko tayari kugombea tena'', amesema Kansela Merkel na kuendelea, ''Uchaguzi huu utakuwa mgumu zaidi kuliko mwingine wowote tuliopitia, kwa sababu tunakumbwa na mgawanyiko mkubwa'' katika jamii.

Kiongozi huyo amebainisha tofauti kati ya Marekani na Ujerumani, akigusia 'vioja' vilivyoziandama kampeni za hivi karibuni kuelekea uchaguzi wa mwanzoni mwa Novemba huko Marekani. Bi Merkel amesema aonavyo yeye, mjadala wa kisiasa unapaswa kuwa wa hoja, badala ya kugombana na kupandikiza chuki.

Amesema kwa Ujerumani, maadili ya demokrasia, uhuru  na heshima kwa haki za binadamu yanapaswa kuwa nguzo za mchakato wa kidemokrasia.

Mwisho wa tetesi

Angela Merkel kandidiert erneut
Wajerumani wengi humtazama Bi Merkel kama nembo ya utengamanoPicha: Getty Images/C. Koall

Tangazo la Bi Angela Merkel limemaliza miezi kadhaa ya tetesi, wakati Ulaya na nchi za Magharibi kwa ujumla zikikabiliwa na kuongezeka kwa umaarufu wa siasa za kuhamasisha hisia za umma.

Kansela Merkel ameiongoza Ujerumani  tangu mwaka 2005, na anapendwa na wapiga kura wanaomtazama kama mtu mwenye kutilia maanani hali halisi ya mambo, mnyenyekevu, na mwenye uongozi ulioivusha salama Ujerumani msukosuko wa mgogoro wa kifedha.

Hata hivyo alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu sera yake ya kuwafungulia milango wakimbizi takriban milioni moja mwaka 2015, ambao walikuwa wamekwama katika nchi za Ukanda wa Balkan.

Kauli mbiu yako kuhusu hatua hiyo, maarufu kama ''Wir Schaffen das'', au ''Twaweza kulifanya hili'', imesababisha mvutano kati yake na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU cha jimboni Bavaria. Sera yake kuhusu wakimbizi pia imekipa umaarufu Chama mbadala kwa Ujerumani, AfD, ambacho kimekuwa kikiuhamasisha umma kwa kuchochea hofu dhidi ya wahamiaji na Waislamu.

Kiongozi wa ulimwengu wa kiliberali

US-Präsident Barack Obama und Bundeskanzlerin Angela Merkel
Obama amemuelezea Kansela Merkel kama ''kiongozi shupavu''Picha: Picture-Alliance/AP Photo/M. Sohn

Hata hivyo, wakati dunia ikielekea katika mwaka mpya unaotabiriwa kuwa na sintofahamu chungu nzima kisiasa, idadi ya Wajerumani wanaotaka Bi Merkel aendelee kushika hatamu za uongozi imekuwa ikiongezeka. Uchunguzi wa maoni uliofanywa Jumapili umeonyesha kuwa asilimia 55 ya Wajerumani bado wanamuunga mkono kiongozi wao, ikilinganishwa na mwezi Agosti ambapo ni asilimia 42 tu waliotaka aendelee kuongoza.

Bi Merkel pia alipigiwa debe sa rais wa Marekani Barack Obama ambaye wiki iliyopita alikuwa ziarani mjini Berlin. Obama alisema Wajerumani hawana budi kumshukuru bi Merkel, na kuongeza kuwa kama angekuwa Mjerumani angeendelea kumuunga mkono.

Alipoulizwa kuhusu dhana iliyopo kwamba sasa yeye ndie kiongozi wa ulimwengu wa kiliberali, Bi Merkel hakunasa katika mtego wa hisia. Jibu lake lilikuwa, ''Hakuna nchi moja inayoweza kivyake, kusuluhisha matatizo yote''.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, ape

Mhariri: Grace Kabogo