Kenya: Vifo kufuatia uunganishaji wa umeme kwa njia haramu
28 Aprili 2021Wakenya wengi wanalalamikia gharama ya juu ya maisha pamoja na kunyanyaswa na kampuni ya umeme nchini humo, licha ya mpango wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme kuonekana kuzaa matunda.
Kampuni ya umeme ya Kenya imetoa tahadhari kwa umma kuhusu uunganishaji wa umeme kinyume cha sheria wanaosema unaendelezwa sehemu nyingi nchini na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Soma pia:Taa za jua zapunguza makali ya umaskini Kenya
Akizungumza mjini Nakuru, Meneja msimamizi wa maswala ya usalama wa kampuni hiyo John Oguda ameeleza kuwa kati ya mwezi Julai mwaka jana na Aprili mwaka huu, watu 93 wamepoteza maisha yao baada ya kurushwa na umeme.
"Tumekuwa na matukio mengi ya uunganishaji haramu wa umeme. Watu wengine pia wanawatumia makanjanja kuwawekea nyaya za umeme. Watu hawafahamu hatari iliyo mbele yao ndiposa kama kampuni tumeamua kuuhamasisha umma,” amesema Oguda.
Mradi wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme
Mwaka 2017 serikali ya Kenya kupitia kampuni ya umeme, ilianzisha mradi wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme uliopewa jina "Last Mile Connectivity”, lengo likiwa kuhakikisha kuwa taasisi zote muhimu kama vile shule na hospitali zimepata umeme.
Soma pia: Kenya, bila nishati hakuna maendeleo
Wakenya walioko maeneo yenye miundo mbinu hafifu kama vile vijijini na maeneo ya mabanda pia ni walengwa kwenye mradi huu. Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa kufikia sasa wameweza kuwafikia Wakenya milioni 34.1 kutoka idadi ya awali ya milioni 12.8.
"Mitaa yetu imekuwa salama kutokana na mradi huu, na wafanyabiashara wanaendeleza kazi zao hata usiku bila uoga. Tunapoendelea kuwaunganisha watu zaidi na umeme tunajenga uchumi wa saa 24 nchini mwetu. Zaidi ya miaka 50 baada ya uhuru wengi wetu waliishi bila umeme kwa sababu ya mipangilio mibovu na dhana potovu,” alisema Rais Kenyatta.
Malalamiko ya ada za juu ya kampuni ya umeme Kenya
Licha ya mafanikio haya Wakenya wamezidi kulalamikia ugumu wa maisha, mara kwa mara kampuni ya umeme ya Kenya ikijikuta inalaumiwa kwa kuwanyanyasa wananchi.
Kwenye mitandao ya kijamii pia, kampuni ya umeme ya Kenya imelaumiwa kwa kutoza ada za juu kupindukia, huduma zisizo madhubuti na uzembe.
Wengine wameelezea kukwera na ukosefu wa ushindani kwenye huduma ya umeme na hata kutishia kugeukia matumizi ya nguvu za nishati ya jua.
Hata hivyo, kampuni ya umeme ya Kenya inaushauri umma kupata mwongozo kutoka kwao ili kuepukana na ajali zaidi.