Korti ya Kijeshi Uganda kumshtaki Besigye kwa usaliti
14 Januari 2025Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, atafikishwa mahakamani kwa kosa zito la usaliti, mahakama ya kijeshi iliamua Jumanne, hatua inayoongeza changamoto za kisheria anazokabiliana nazo kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwaka 2026. Kosa la usaliti lina adhabu ya kifo kwa wanaopatikana na hatia.
Besigye, ambaye amegombea urais mara nne, alitoweka jijini Nairobi, Kenya, Novemba 16. Siku chache baadaye, yeye na msaidizi wake, Obeid Lutale, walifikishwa mahakamani mbele ya mahakama ya kijeshi jijini Kampala, mji mkuu wa Uganda.
Besigye alishtakiwa kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na kwa tuhuma za kuomba msaada wa kijeshi kutoka nje kwa lengo la kuvuruga usalama wa taifa. Besigye, aliyekanusha mashtaka hayo, amewekwa rumande tangu wakati huo.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi Jumatatu alibadilisha hati ya mashtaka na kuongeza shtaka la usaliti pamoja na kumtaja mshukiwa wa tatu, ambaye ni afisa wa jeshi, hatua iliyowashangaza mawakili wa utetezi waliopinga mabadiliko hayo.
Besigye, mwenye umri wa miaka 68, amekamatwa na kushambuliwa mara nyingi katika maisha yake ya kisiasa lakini hajawahi kupatikana na hatia ya uhalifu.
Hofu ya mabadiliko ya kisiasa Uganda
Shirika la kutetea haki za binadamu , Amnesty International limetoa wito wa kuachiliwa kwake, likisema "utekaji wake ulikiuka wazi sheria za kimataifa za haki za binadamu na mchakato wa kuhamishwa pamoja na haki za msingi za kesi ya haki."
Soma pia: Martha Karua Kumtetea Dkt Kizza Besigye katika mahakama ya kijeshi Uganda.
Kwa mujibu wa Human Rights Watch, kesi ya Besigye ni "mfano wa hivi karibuni wa mamlaka ya Uganda kutumia vibaya mahakama za kijeshi na mashtaka yanayohusiana na jeshi ili kukandamiza upinzani." Kesi hiyo inafuatiliwa kwa karibu na wananchi wa Uganda wanaohofia mabadiliko ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa urais.
Ingawa Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, anatarajiwa kugombea tena, baadhi ya wachambuzi wanaamini huenda akastaafu. Museveni hana mrithi dhahiri ndani ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), hali inayochochea hofu kubwa kuhusu mabadiliko yasiyotarajiwa ya kisiasa.
Besigye, ambaye ni daktari wa tiba na aliehudumu katika jeshi la Uganda akiwa na cheo cha kanali, ni rais wa zamani wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC).
Akiwa kiongozi wa FDC, chama hicho kilikuwa kwa miaka mingi chama kikuu cha upinzani nchini Uganda. Yeye ni mkosoaji mkubwa wa Museveni, ambaye aliwahi kumhudumia kama msaidizi wa kijeshi na daktari binafsi kabla ya kutofautiana naye miaka ya 1990 kutokana na kile alichosema ni mwelekeo wa Museveni wa udikteta.
Soma pia: Wapinzani Uganda waungana kumkabili Museveni 2026
Kwa muda mrefu, Museveni amekuwa akikosolewa na mashirika ya haki za binadamu kwa madai ya ukiukaji dhidi ya viongozi wa upinzani. Uganda haijawahi kushuhudia mabadiliko ya madaraka kwa amani tangu ilipopata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza mwaka 1962.
Chanzo: AFP