1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Krejeshwa nyumbani Magaidi wa IS Magazetini

Oumilkheir Hamidou
19 Februari 2019

Wito wa rais Donald Trump wa Marekani kutaka magaidi wa IS wajereshwe katika nchi walikotokea na kitisho chake cha kuyawekea makampuni ya magari ya Ulaya ushuru ziada ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/3Ddw9
Syrien Baghus  - Frauen fliehen mit ihren Kindern aus dem IS-Dorf
Picha: picture-alliance/dpa/A. Hamam

Mada mbili kuu zimegonga vichwa vya magazeti ya Ujerumani na zote zimechochewa na rais Donald Trump wa Marekani:  Kwanza wito wa Rais wa Marekani Donald Trump aliyewataka viongozi wa Ulaya wawarejeshe nyumbani raia wao waliokuwa wakipigana upande wa wanamgambo wa itikadi kali wa kile wanachokiita Dola la Kiislamu, IS, nchini Syria na pili ni kitisho cha huyo huyo rais wa Marekani cha kuyatoza ushuru ili kuyaadhibu makampuni ya Ulaya  yanayotengeneza magari.

Tunaanza na mjadala uliopamba moto kuhusu madai ya kurejeshwa nyumbani wanamgambo wa IS wanaoshikiliwa na wapiganaji wa kikurd nchini Syria. Maoni ni tofauti magazetini kuhusu suala hilo. Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika: "Bila ya shaka viongozi wa mjini Washington hawajakosea linapohusika suala la kurejeshwa nyumbani wapiganaji hao wa kigaidi wa IS. Lakini kwa hisani yenu sio kwa sauti hiyo ya kuamrisha."

Si vyema kuwatwika wakurd mzigo peke yao

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linahisi Donald Trump hajakosea alipozitaka nchi za Ulaya ziwarejeshe nyumbani raia wao wanaoshikiliwa na wapiganaji wa kikurd nchini Syria. Gazeti linaandika: "Ndio Rais Trump kafanya vizuri angalau kwa kuwataka viongozi wa Ulaya wawarejeshe nyumbani raia wao waliokuwa wakiwasaidia magaidi wa IS. Kwasababu haitokuwa sawa kuwaachia wakurd waliolazimika kwanza kupambana na magaidi wa IS na kuokoa maisha ya maelfu ya raia, waubebe peke yao pia mzigo wa wanamgambo hao wa itikadi kali. Ulaya hapo haistahiki kukaa kimya. Na zaidi ya hayo kila halifu hata kama ni gaidi mtuhumiwa ana haki ya kufunguliwa kesi ambayo  itakuwa ya haki. Kesi kama hiyo haitowezekana si nchini Syria na utawala wa kiimla wa Assad na wala si katika maeneo ya utawala wa ndani wa wakurd ambako mfumo wa dola linaloheshimu sheria ndio kwanza unaanzishwa."

 

Waatuhumiwa wahukumiwe kuambatana na sheria

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten lina maoni sawa na hayo na kuandika: "Mwenye kufanya uhalifu lazma ahukumiwe. Na hilo linabidi lifuate msingi wa kimataifa. Nchini Syria lakini hakuna sheria inayostahiki jina hilo. Wahalifu kuwafikisha mahakamani katika nchi ambako wana uraia ni jambo linalostahiki kuzingatiwa hata kama si rahisi. Kutahitajika mtuhumiwa na pia chanzo.

Hali ya kuvunjika moyo haitoepukika na hapo hata kabla ya shughuli zenyewe za kisheria kuanza. Lakini hakuna njia nyengine. Au watu waziachie taasisi za kisheria za Syria zisimamie kesi hizo? Haiingii akilini. Na haingii akilini hata kidogo pia kuyafumbia macho yaliyotokea. Kilichosalia ni kuzipatia fedha zaidi taasisi za kisheria ili kuweza kukabailiana na jukumu jipya."

Ushurun wa ziada wa rais Trump unawreza kumgeukia

Mada ya mwisho magazetini inahusu vitisho vya rais Trump kuyawekea ushuru ziada makampuni ya magari ya nchi za ulaya. Gazeti la Rheinpfalz linaandika:"Bila ya shaka sio usalama wa taifa unaomshughulisha zaidi rais Trump. Kwa kuyatoza makampuni ya magari ya Ulaya ushuru ziada anataka tu kusababisha bei zipande katika masoko ya Marekani ili wanunuzi wayageukie zaidi magari yaliyotengenezwa Marekani. Kama hesabu hizo zitaleta tija, hakuna uhakika. KIlicho na uhakika lakini ni kwamba pindi rais Trump akiamua kweli kutangaza ushuru ziada, basi nchi za Ulaya nazo hazitokaa kimya, zitajibisha.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef