1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake

Mohamed Dahman8 Machi 2007

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo ni leo hii Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetowa wito wa kukomeshwa kwa vitendo vyote vya matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake na wasichana katika mizozo yenye kuhusisha matumizi ya silaha.Wakati siku hii ikiadhimishwa imebainishwa kwamba wanawake bado wameachwa nyuma katika masuala ya ajira.

https://p.dw.com/p/CB5O
Wanawake nchini Rwanda
Wanawake nchini RwandaPicha: picture-alliance/ dpa

Katika mkesha wa kuamkia siku hii ya wanawake duniani baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la nchi wanachama 15 limepitisha azimio lisiloshurutisha linaloaani kuenea kwa aina zote za matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake na wasichana katika mizozo yenye kuhusisha matumizi ya silaha ikiwa ni pamoja na mauaji,kuwatia vilema,kuwaingilia kingono kwa nguvu,utekaji nyara na kuwasafirisha kwa njia ya magendo.

Azimio hilo linataka wahusika wote katika mizozo kuchukuwa hatua mahsusi kuwalinda wanawake na wasichana kutokana na ukatili wa kijinsia hususan ubakaji na dhuluma nyenginezo za ngono.

Baraza hilo la Usalama limesisitiza kuwajibika kwa mataifa yote kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika na mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa vita ikiwa ni pamoja na ule unaohusiana na ngono na matumizi mengine ya nguvu dhidi ya wanawake na wasichana.Pia limeyakinisha umuhimu wa dhima ya wanawake katika kuzuwiya na kusuluhisha mizozo na katika kuleta amani,haja ya kuwashirikisha na kuwahusisha kikamilifu katika juhudi zote za kudumisha amani na usalama.

Halikadhalika baraza la usalama limezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuongeza uwakilishi wa wanawake katika ngazi zote za kutowa maamuzi katika taasisi za taifa,kanda na za kimataifa na katika utaratibu wa kuzuwiya, kudhibiti na kutatuwa mizozo.

Mapema katika ujumbe wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon amesema matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake yanaendelea bila ya kudhibitiwa katika kila bara,nchi na tamaduni kwa sababu mara nyingi hufichwa au huridhiwa kimya kimya.

Ban ameilezea siku ya kimataifa ya wanawake kuwa ni fursa kwa wanawake na wanaume kuungana katika mapambano ambayo yanawahusisha binaadamu wote.

Amesema kuwawezesha wanawake sio lengo kama lenyewe lilivyo bali ni sharti kwa ajili ya kujenga maisha bora kwa kila mtu duniani.

Repoti ya Shirika la Kazi la Kimataifa ILO iliotolewa wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake imesema wanawake wamekuwa wakijiunga na guvu kazi kwa idadi kubwa kabisa lakini bado hawalipwi sawa na wanaume,hawaelimishwi vya kutosha na huwa rahisi zaidi kutimuliwa kazini na kwamba ubaguzi ukijumuishwa pamoja na idadi inayoongezeka ya wanawake makazini kumepelekea kunenea kwa umaskini wa wafanyakazi wa kike.

Mkuu wa ILO Juan Somavia amesema licha ya kupigwa kwa hatua fulani wanawake bado wamekwama kwenye ajira za kipato cha chini mara nyingi katika sekta zisizo rasmi wakiwa hawana kinga ya kutosha ya kisheria,wana kinga ndogo ya kijamii na ukosefu wa usalama wa kiwango kikubwa kabisa.

Wanawake bilioni 1.2 wamekuwa wakifanya kazi hapo mwaka jana kati ya nguvu kazi ya watu bilioni 2.9 duniani na hufanya asilimia 60 ya wafanyakazi wa kimaskini duniani au wale ambao hulipwa pungufu ya dola moja kwa siku.