1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya wanawake yapaza sauti

P.Martin21 Septemba 2007

Sauti zinazidi kupazwa kuwapa wanawake nafasi ya kushirikiana zaidi katika maamuzi ya kupanga sera,huku viongozi wakijitayarisha kuhudhuria mkutano wa kimataifa mjini New York kujadili mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/CB17

Viongozi hao wa kimataifa,wanakutana Jumatatu ijayo mjini New York,kufanya matayarisho ya mkutano wa kilele utakaofanywa Bali nchini Indonesia katika mwezi wa Desemba,kujadili tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Lakini viongozi wa kike wanaowakilisha makundi mengi ya jamii za kiraia wanasema,serikali nyingi kwa sehemu kubwa,zimeshindwa kutia maanani vipi wanawake wanavyoathirika na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa maoni ya WEDO-Shirikisho la Wanawake kuhusika na Mazingira na Maendeleo,ni wanawake wanaoteseka kuliko wanaume maafa yanapotokea.Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kuwa wanaume na wanawake wanaathirika tofauti,yanapotokea maafa ya kimaumbile na mabadiliko ya hali ya hewa.Sababu ni kuwa mara nyingi,msingi wa majukumu yao hauna usawa.

Kwa hivyo leo Ijumaa viongozi wa kike wanaowakilisha jamii za kiraia,wanakutana kabla ya mkutano wa Jumatatu,ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Majadiliano ya makundi ya jamii za kiraia,yanaongozwa na rais wa zamani wa Ireland,Mary Robinson na aliekuwa waziri mkuu wa Norway,Gro Harlem Brundtland.Wote wawili wanaheshimiwa katika jumuiya ya kimataifa kwa juhudi zao za kugombea haki za binadamu na mazingira.

Lengo la majadiliano hayo ni kuhakikisha kuwa uamuzi utakaopitishwa kwenye mkutano wa Katibu Mkuu utazingatia matatizo yanayokabiliwa na wanawake kuhusika na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na majukumu ya wanawake kudhibiti athari hizo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa WEDO,Bibi June Zeitlin,wanawake wanaoishi katika nchi zinazoendelea wanakumbana na vikwazo vikubwa zaidi.Anasema,licha ya kuwepo makubaliano ya kimataifa,kuwashirikisha wanawake sawasawa,bado katika nchi nyingi sana wanawake wanaendelea kutengwa,maamuzi yanapopitishwa.

Wanaharakati wa kike wanasema,majadiliano yanayofanywa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani,yanazigatia zaidi suala la kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochafua mazingira badala ya matatizo ya kijamii na ustawi wa jumuiya. Taarifa ya pamoja iliyotolewa na makundi mbali mbali ya wanawake inasema,Katibu Mkuu,Ban Ki-Moon anapaswa kutoa ujumbe imara wa kufungamanisha usawa wa jinsia katika maamuzi yatakayopitishwa kwenye mkutano wa Bali.