1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni kuhusu kashfa ya rais wa benki ya dunia

18 Mei 2007

Bara Ulaya limepokea habari za kung’oka kutoka madarakani rais wa benki ya dunia Paul Wolfowitz kwa faraja kubwa huku nchi hizo zikihimiza hatua za haraka zifanyike kumchagua rais mpya.

https://p.dw.com/p/CB43
Paul Wolfowitz rais wa benki ya Dunia
Paul Wolfowitz rais wa benki ya DuniaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Uingereza imesisitiza msimamo wake wa kuiunga mkono benki ya dunia na wakati huo huo imesema imefarijika kuwa wakati mgumu ulioikabili taasisi hiyo ya fedha ya kimataifa sasa umefikia kikomo.

Taarifa hiyo imetolewa rasmi na waziri wa maendeleo ya kimataifa wa Uingereza bwana Hilary Benn kufuatia tangazo la kujiuzulu kwa kinara wa benki ya dunia Paul Wolfowitz baada ya kubanwa na shinikizo za kumtaka aachie ngazi kutokana na kashfa ya kumuoengezea kitita cha fedha mpenzi wake ambae pia ni mfanyakazi wa benki ya dunia.

Wakati huo huo mashirika ya kutoa misaada ya Uingereza yamemtaka waziri mkuu anae ondoka Tony Blair na waziri mkuu mtarajiwa Gordon Brown kuunga mkono mwito wa kupinga mfumo wa kumchagua rais wa benki kuu ambao kila mara unapendelea raia wa Marekani.

Seneta Christopher Dodd mmoja kati ya wagombea wa kiti cha urais wa chama cha Demoktratik nchini Marekani amesema kitendo cha bwana Wolfowitz kinaifanya taasisi hiyo ya kimatiafa itiliwe shaka juu ya kutimiza jukumu la kupambana umasikini duniani.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrueck amesema, ni bora mtu ajiuzulu kutoka kwenye cheo muhimu kama hicho ili kulinda hadhi yake na pia hadhi ya taasisi.

Amesema inabidi benki ya dunia isiangalie nyuma bali indelee mbele kufanya kazi zake na kujenga uaminifu wake kwani benki hiyo ni muhimu sana kwa nchi zinazo endelea.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels imeelezea uhusiano mzuri uliokuwepo baina ya kamishseni hiyo na bwana Wolfowitz lakini hata hivyo imehimiza jitihada za haraka ili kumchagua rais mpya wa taasisi hiyo ya kimataifa.

Japan ambayo ni nchi muhimu inayoshika nafasi ya pili baada ya Marekani kwa katika umiliki wa hisa na ufadhili wa benki ya dunia, imesema swala la kumteuwa rais mpya wa tasisi hiyo ya kimatiafa ni jukumu la benki hiyo ya dunia.

Bwana Daniel Owen kutoka kitengo cha maendeleo ya jamii katika benki ya dunia amesema alipokuwa safarini katika Afrika ya magharibi alishuhudia jinsi mzozo wa bwana Wolfowitz ulivyoleta dharuba kubwa katika taasisi hiyo ya kimataifa hususan katika sera za utawala bora ambazo zinasisitizwa sana na benki ya dunia.

Wachambuzi kutoka barani Afrika wanasema kashfa ya Wolfowitz itaathiri vibaya hadhi ya benki ya dunia barani humo.

Waziri wa wa habari wa Zambia Mike Mlongotí amesema bara la Afrika ni washirika muhimu wa benki ya dunia.

Ingawa Afrika haina usemi katika maamuzi ya kuchagua kinara wa benki ya dunia lakini bara hilo ndilo linakumbwa zaidi na masharti magumu ya taasisi hiyo ya kimatiafa.