Maoni: Merkel, tafadhali onyesha hisia zaidi!
29 Julai 2016Ni jambo linalojulikana kwamba Kansela huyo wa Ujerumani sio mtu wa kutowa hotuba zilizojaa hisia kwa hiyo kuhusiana na suala hilo tangazo lililotolewa na vyombo vya habari kadhaa nchini Ujerumani kwamba Angela Merkel "kulihutubia taifa lilikuwa linapotosha.
Kama vile siku zote inavyokuwa katika kadhia kama hizo alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa ulinganisho na uchambuzi.Ziada ya hayo safari hii utaratkibu ulikuwa tafauti ambapo mkutano wake na waandishi wa habari unaofanyika kila mwaka katika majira ya kiangazi mjini Berlin umesogezwa mbele kutokana na mashambulizi kadhaa ya kutumia nguvu yaliofanyika Ujerumani siku chache zilizopita.
Hata hivyo matarajio yaliokuwa yamewekewa mkutano wake huo yalikuwa tafauti kulinganisha na yale ya miaka iliopita.Mashambulizi ya kwanza ya kigaidi kufanyika ndani ya nchi yao wenyewe kumewaudhi Wajerumani wengi na kusababisha hofu na kuzusha masuala mengi.
Mojapo ya masuala muhimu je ulikuwa ni uamuzi mzuri kuwaingiza nchini wakimbizi wengi bila ya kuwa na udhibiti kamili wa wimbi hilo kubwa kuanzia mwanzo?Sio tu watu wanaotumia mitandao ya kijamii wana wasi wasi na hali hiyo bali hata mtu wa kawaida kabisa, mfanyakazi au hata wananchi wanaoishi vijijini pia walikuwa na mashaka yao kwa hilo.
Ingawa sio wote lakini ni wengi tu ukiachia mbali wapinzani wa kisiasa wa sera ya Merkel kutoka chama cha sera kali za mrengo wa kulia chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD).
Masuala mengi yahitaji majibu
Wakati wa hotuba yake hiyo ya dakika 90 na waandishi wa habari Merkel aliacha masuala mengi yanayohitaji majibu kuhusiana na kushughulikia mashaka yao hayo.
Yumkini ikawa ni sahihi kwa wanasiasa kutoongozwa na jazba kama vile alivyoeleza na kwamba hatua kadhaa kubwa zilikuwa zinahitajika kuchukuliwa kukabiliana na changamoto ngumu. Pia ni kweli kwamba hatua nyingi zimechukuliwa kuziweka sera za kuomba hifadhi za Ujerumani na Ulaya katika msingi mpya endelevu.
Hata hivyo katika nyakati kama hizo Merkel angelikuwa ameshauriwa vyema kuonyesha hisia fulan ,ni fursa ambayo imepotezwa.Kinachokosekana katika hotuba yake hiyo na majibu kwa waandishi wa habari ni madaraja ambayo angelistahiki kuyajenga kuzuwiya kuongezeka kwa pengo la kugawanyika kati ya watu wanaotetea na wanaopinga sera yake ya wakimbizi.
Safari hii alitakiwa awe amegonga ngumi mezani kwa vitendo ili kutowa ishara kwamba "basi inatosha ....inatosha!".Mpango wake wa usalama wa vipengele tisa alioutambulisha kwa wananchi ni dhaifu na haukuwafikia walengwa.
Mwandishi: Kay- Alexander Scholz/Mohamed Dahman
Mhariri: Yusuf Saumu