Maoni:Cyprus yakabiliwa na wakati mgumu
25 Machi 2013Cyprus haijafilisika, lakini italazimika kuachana na mitindo iliyokuwa ikiendelea hadi sasa na shughuli zake za kiuchumi zitadorora.
Maelfu ya nafasi za kazi katika sekta ya shughuli za fedha zitapotea, kwani sekta hiyo ndiyo inayowaajiri zaidi ya nusu ya wafanyakazi katika kisiwa hicho cha Bahari ya Kati.
Yote hayo yameshapita, kwani licha ya serikali ya Cyprus kujaribu kwa muda mrefu kuzinusuru benki zake, haikufanikiwa.
Bila ya shaka, Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya fedha, Olli Rehn, hajakosea aliposema kwamba Cyprus inaelekea katika kipindi kigumu.
Siku ngumu ndio zinaanza sasa
Mnamo miezi na miaka inayokuja, fedha za walipa kodi zinapungua na zile za huduma ya jamii zitaongezeka. Tangu sasa mtu anaweza kuashiria kwamba msaada uliokubaliwa wa Euro bilioni 10 hautotosha kukidhi bajeti ya serikali.
Mwenyekiti wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Christine Lagarde, hakufafanua aliposema madeni ya Cyprus hata mwaka 2020 yatakuwa asilimia 100 ya nguvu za kiuchumi za nchi hiyo.
Kama wakaazi 800,000 wa Cyprus wataweza kuutwaa mzigo huo, hakuna ajuae. La kuhofia ni ile hali kwamba wawekezaji wa kigeni, Warusi sawa na Wagiriki, wakibeba fedha zao wanaanza kukihama kisiwa hicho. Cyprus inaweza kwa muda mrefu kugeuka mtihani unaohitaji marekebisho wa Umoja wa Ulaya.
Mpango wa kuiokoa Cyprus kama ulivyofikiwa usiku wa manane wa kuamkia Jumatatu (25 Machi), umezusha ufa mkubwa katika juhudi za kupambana na mgogoro wa Euro unaozidi makali.
Wateja wa benki wabebeshwa mzigo mzito
Kwa mara ya kwanza wateja wa benki wanalazimishwa kutoa fedha kuziokoa benki ambazo zinakaribia ukingoni mwa kufilisika. Mteja yeyote yule wa benki ya pili kwa ukubwa nchini Cyprus, Laiki Bank, aliyeweka akiba ya zaidi ya euro 100,000 atajikuta akipoteza sehemu kubwa ya pesa zake.
Benki hiyo sasa inafungwa. Onyo kwa wateja wa benki barani Ulaya ni kwamba pesa zenu haziko salama kokote kule kwa sababu ikiwa nchi inakaribia kufilisika, basi pesa zenu zitachukuliwa.
Onyo pia kwa benki ni kwamba taasisi inayocheza kamari katika masoko ya hisa haina nafasi kubwa ya kuokolewa kama ilivyotokea katika kadhia kama hiyo nchini Ugiriki, Ireland na Hispania.
Hapa lakini kuna kikomo
Laiki Bank inamilikiwa kwa sehemu kubwa na serikali ya Cyprus. Kwa hivyo, taifa la Cyprus linapoteza pesa ambazo kwa upande wa pili linazipata kupitia mkopo kutoka kwa mataifa yaliyosalia ya Umoja wa Ulaya na IMF.
Miongoni mwa wateja wakubwa wa Laiki Bank ni mashirika kadhaa ya bima ya uzeeni kisiwani humo, lakini hakuna ajuaye ikiwa zile euro bilioni 4.2 zilizoahidiwa zipatikana kwa kuvunjwa benki hiyo.
Benki Kuu ya Ulaya haimo katika kizungumkuti hicho. Madai yake ya euro bilioni 9 kwa benki ya Laiki yametwikwa Benki Kuu ya Cyprus. Mkopo unaotolewa na Benki Kuu ya Ulaya na kwa namna hiyo na walipa kodi wote wa nchi za kanda ya Euro zitatumika kwa namna yoyote ile.
Hasara kwa Cyprus kubakia kwenye euro
Cyprus inaigharimu mengi kuweza kusalia katika umoja wa sarafu. Kwa mtazamo wa kiuchumi lingekuwa pengine jambo la busara kwa nchi ndogo kama hii kujitoa katika Umoja huo na kuanza kutumia sarafu iliyopunguzwa thamani yake.
Mataifa 16 yatakayosalia ya Umoja wa Ulaya yasingekubali hatua hiyo. Yanahofia hali hiyo isije ikadhoofisha nguvu za sarafu yao ya euro na sifa ya sarafu hiyo ulimwenguni. Hakuna anaeweza kuashiria madhara ya kujitoa Cyprus katika umoja wa sarafu hiyo.
Kwamba mkakati wa kukabiliana na mgogoro tangu katika kanda ya euro mpaka katika serikali ya Cyprus haukuwa mzuri, kila mmoja anakubaliana na ukweli huo. Vuta nikuvute iliyoshuhudiwa miezi iliyopita ilikuwa kazi bure - imevuruga imani ndani na nje ya kanda ya euro.
Mfumo wa benki za Cyprus ulikuwa umeoza na hakuna ambae angeweza kuzinusuru. Na hilo lilikuwa likijulikana tangu Juni 2012, pale Cyprus, kutokana na hasara iliyoipata kutokana na mpango wa kuinusuru Ugiriki, ilipoomba kwa mara ya kwanza isaidiwe.
Cyprus, Umoja wa Ulaya wote walikosea
Serikali ya Cyprus ilivuta muda kuanzisha mazungumzo, Nazo nchi za kanda ya euro zilikuwa zikiringa. Ilibidi kwanza Benki Kuu ya Ulaya kutishia kuifungia Cyprus njia za kupata fedha ndipo watu walipoanza kuzindukana.
Yadhihirika, kwa hivyo, kwamba Benki Kuu ya Ulaya ndiyo yenye usemi na sio mawaziri wa fedha. Hilo si jambo la maana. Kwa sababu nani anaidhibiti Benki Kuu ya Ulaya? Mabunge nchini Ujerumani, Uholanzi na Finland yanabidi kimsingi yaidhinishe makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Cyprus.
Hilo bila ya shaka litafanyika.Bunge la Cyprus hata halitoulizwa maoni yake pengine. Hilo litazidisha hasira na ghadhabu za baadhi ya wabunge wa Cyprus dhidi ya Ulaya. Lakini hawana njia nyengine.
Urusi imeiacha mkono Cyprus maji yalipozidi unga. Hivi sasa Wacyprus wanalazimika ama kutekeleza masharti yaliyopitishwa au kujitoa katika kanda ya euro.
Mwandishi: Bernd Riegert
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Mohammed Khelef