1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano ya Hodeida yazusha hofu ya mgogoro wa kibinaadamu

19 Septemba 2018

Hofu inaongezeka ya kuzuka mgogoro zaidi wa kibinaadamu nchini Yemen baada ya wanajeshi wa serikali wakisaidiwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kufanya msururu wa mashambulizi Hodeida

https://p.dw.com/p/358MD
Yemen Sanaa - Kinder erhalten essen
Picha: picture-alliance/dpa/XinHua/M. Mohammed

Hayo ni wakati shirika la hisani la Save the Children likionya leo kuwa Zaidi ya watoto milioni tano wanakabiliwa na kitisho cha njaa katika taifa hilo lililoharibiwa na vita. 

Waasi wa Houthi wanaituhumu serikali na washirika wake wanaoongozwa na Saudi Arabia kwa kuyalenga makusudi maghala ya chakula wakati muungano huo wa kijeshi ukisema kuwa umeanzisha tena operesheni ya kijeshi ili kuukomboa mji wa Hodeida na bandari yake.

Wanajeshi wanaoiunga mkono serikali na duru za madaktari katika mkoa wa Hodeida zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Wahuthi 40 waliuawa karibu na mji huo unakabiliwa na mashambulizi tangu jana usiku.

Umoja wa Mataifa ulionya kuwa mapigano yoyote makubwa huenda yakasitisha utoaji wa chakula kwa Wayemen milioni nane wanaotegemea msaada ili kuishi.

Yemen - al-Hudaida
Hodeida ni muhimu katika kuingiza bidhaa YemenPicha: picture-alliance/afk-images/H. Chapollion

Nalo shirika la hisani la Save The Children limesema leo katika ripoti kuwa kuvurugwa misaada inayoingia Yemen kupitia Hodeida huenda kukasababisha kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha watu kuteseka kwa njaa.

Limesema watoto milioni moja Zaidi sasa wanakabiliwa na kitisho cha njaa wakati bei za vyakula na mafuta zikipanda, na kufikia jumla watoto milioni 5.2.

Kiongozi Baraza Kuu la Mapinduzi la waasi Mohammed Ali al-Huthi amesema maghala ya chakula cha msaada wa kimataifa yalilengwa katika mashambulizi ya Hodeida.

Msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia hajazungumzia huku msemaji wa Shirika la Chakula Duniani – WFP akikataa kusema kama vituo vya shirika hilo la Umoja wa Mataifa vilishambuliwa au la.

Saudi Arabia na washirika wake wanawatuhumu waasi wa Houthi kuwa wanaingiza silaha kutoka Iran kupitia Hodeida, madai ambayo waasi hao pamoja na Iran wanakanusha, na wameweka mzingiro katika bandari hiyo

Genf UN Jemen Sonderbeauftragter Martin Griffiths
Griffiths yuko Riyadh kwa ziara ya siku tatuPicha: Reuters/D. Balibouse

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anatarajiwa kuwasili mjini Riyadh leo, baada ya kuondoka katika mji mkuu wa Yemen Sanaa kwa ziara ya siku tatu.

Griffiths anashinikiza kuanzishwa kwa mazungumzo mapya ya Amani baada ya mazungumzo ya Geneva kushindwa kuanza, huku Wahuthi wakisema kuwa hawakupewa hakikisho la kurudi nyumbani salama baada ya mazungumzo.

Umoja wa Mataifa umesema unaweka utaratibu wa kuwasafirisha kwa ndege hadi ng'ambo wagonjwa wa saratani nchini Yemen. Lakini Wahuthi wamesema mipango hiyo ilisitishwa na jeshi la muungano katika mji wa waasi wa Sanaa wakilituhumu kwa kutoshirikiana

Msemaji wa Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, Fadela Chaib ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hakuna tarehe iliyowekwa ya kufanyika safari ya kwanza hadi pale pande zote zikapoidhinisha.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi