1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais Tshisekedi, Kagame kufanya mazungumzo ya amani Angola

13 Desemba 2024

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wanatarajiwa kukutana Jumapili nchini Angola

https://p.dw.com/p/4o5lU
Marais Felix Tshisekedi | João Lourenço | Paul Kagame
Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na rais wa rwanda Paul Kagame (kulia) wamethibitisha watashiriki mkutano huo

Mkutano huo ni awamu mpya ya mazungumzo yanayodhamiria kuumaliza mzozo wa Mashariki mwa Kongo.

Rwanda imethibitisha ushiriki wa Kagame atakayeambatana na Waziri wake wa Mambo ya Nje Olivier Nduhungirehe.

Kwa upande wake Rais Tshisekedi atahudhuria mazungumzo hayo licha ya kukataa hapo awali kuzungumza na Rwanda na kutoa wito uliotaka nchi hiyo jirani kuwekewa vikwazo vya kimataifa. 

Mwenyeji wa mazungumzo hayo Rais wa Angola Joao Lourenco, aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa msuluhishi amesema hapo jana kuwa ana matumaini kwamba mazungumzo yatakayofanyika mjini Luanda yatawezesha kufikiwa  makubaliano ya amani ya kudumu kati ya Kongo na Rwanda. 

Hivi karibuni, Rwanda na DRC zilitia saini nyaraka muhimu kwa ajili ya kuendeleza mchakato huo wa amani mashariki mwa Kongo, eneo linalokumbwa na uasi wa makundi kadhaa yenye silaha.