1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMsumbiji

Marekani, Uingereza na wengine walaani machafuko ya Msumbiji

28 Novemba 2024

Serikali za Marekani, Uingereza, Canada, Norway na Uswisi zimelaani kwa pamoja ghasia zinazoongezeka dhidi ya raia nchini Msumbiji, baada ya taifa hilo la kusini mwa Afrika kugubikwa na maandamano ya baada ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4nWUJ
Mosambik | Maandamano ya kupinga ushindi wa chama tawala
Marekani, Uingereza na wengine walaani kuongezeka kwa machafuko MsumbijiPicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Taarifa ya madola hayo makubwa imeitaka serikali ya Msumbuji kuzingatia jukumu la vikosi vya usalama na kuwalinda watu wa Msumbuji.

Hasira ya umma imeongezeka baada ya matokeo ya uchaguzi wenye utata wa mwezi uliopita, ambayo yalizusha maandamano kutoka kwa wafuasi wa upinzani. Chama cha Frelimo kilishinda uchaguzi huo na kurefusha utawala wake wa miongo mitano huku mgombea wake, Daniel Chapo, akimrithi Rais Filipe Nyusi kuwa rais wa tano wa Msumbiji tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno.

Shirika la HRW: Askari wa Msumbiji wamewaua watoto 10

Upinzani ukiongozwa na mgombea mkuu Venancio Mondlane unapinga kile unachosema ni ushindi wa udanganyifu wa Frelimo, chama ambacho kimetawala Msumbiji tangu 1975.

Waandamanaji jana walikabiliana na vikosi vya usalama kote Msumbiji huku polisi ikiripotiwa kuwauwa watu wawili. Aidha, gari la kijeshi lilimgonga na kumuuwa mtu mwingine katika maandamano hayo ya kupinga uchaguzi wa Oktoba 9.