1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yafuta mkataba wa kuiuzia silaha Saudi Arabia

14 Desemba 2016

Serikali ya rais Barack Obama imefutilia mbali mkataba wa kuiuzia Saudi Arabia baadhi ya silaha. Hatua hiyo ni ishara ya kupinga kampeni ya mshirika wake huyo nchini Yemen ambayo imesababisha mauaji ya raia wengi.

https://p.dw.com/p/2UFCD
Jemen Zerstörung in Straße von Taiz
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Basha

Utawala wa Rais Barack Obama umeamua kutowauzia baadhi ya silaha Saudi Arabia ambayo ni moja kati ya nchi washirika wa Marekani. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa cheo cha juu mjini Washington, ushirikiano wa masuala ya usalama sio kitu cha mchezo na kwamba Marekani imeamua kutokuendelea na uuzaji wa vifaa vya kijeshi kwa Saudi Arabia kutokana na taifa hilo kubwa kutoridhika na jinsi Saudi Arabia inavyoendelea kufanya makosa katika operesheni yake ya anga nchini Yemen.  

Wakati huo huo miili 11 ya watu imepatikana imetupwa katika hifadhi. Miili hiyo ya wanaume ambayo ilikuwa haina vichwa imepatikana imetupwa katika hifadhi ya al-Hiswa iliyopo magharibi ya mji wa Aden. Ingawa taarifa kamili kuhusiana na mauaji hayo bado hazijatolewa lakini gazeti la Aden la al-Ghad limeripoti kwamba miili hiyo ilitupwa mahala hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja. 
Mji wa Aden wa pili kwa ukubwa nchini Yemen umekumbwa na visa vya uvunjaji sheria wakati ambapo makundi yaliyojihami kwa silaha kama kundi linalojiita dola la Kiislamu IS na kundi la kigaidi la al Qaeda yanaendelea kuwa na nguvu katika kipindi chote cha mwaka mmoja na nusu baada ya wafuasi wa Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi kulifurusha kundi la Houthi lililokuwa linaungwa mkono na majeshi ya ushirika wa nchi za kiarabu. Takriban watu elfu 10 wameuwawa katika machafuko hayo yaliyodumu kwa miezi 20 na ambayo yamesababisha hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo masikini.
Juu ya watu wanne waliouwawa katika mashambulizi ya hivi karibuni nchini Yemen, watu watatu walikuwa watuhumiwa wa kundi la kigaidi la Al Qaeda na mmoja alikuwa ni kamanda wote waliuwawa baada ya gari walilokuwemo kushambuliwa na ndege isiyo na rubani mashariki ya mji mkuu wa Sanaa. Inaaminika kuwa ndege hiyo isiyo na rubani ilikuwa ya Kimarekani.

Jemen Präsident Abed Rabbo Mansur Hadi
Rais Abd Rabbu Mansour Hadi wa YemenPicha: Reuters/F. Al Nasser

Marekani imethibitisha kutumia ndege zake hizo zisizo na rubani katika mapambano dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kiislamu wenye msimamo mkali nchini Yemen lakini imekuwa haisemi pale ndege zake hizo zinapotumiwa kufanya mashambulio.

Mwandishi:  Zainab Aziz/AFPE/RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo