1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka mapigano kusitishwa Yemen

Caro Robi
31 Oktoba 2018

Marekani imetaka kusitishwa mapigano nchini Yemen na kufanyika mazungumzo ya amani huku muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukiyatuma majeshi 10,000 zaidi kuelekea mji wa Hodeida unaodhibitiwa na waasi.

https://p.dw.com/p/37Pto
Jemen - Hungersnot
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Mohammed

Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis ametaka kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Yemen na pande zinazozana kufanya mazungumzo katika kipindi cha siku thelathini zijazo.

Mattis amesema Marekani imekuwa ikiutizama mzozo wa Yemen kwa muda wa kutosha na anaamini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ni washirika muhimu wa muungano wa kijeshi unaoungwa mkono na Marekani dhidi ya waasi wa Houthi wako tayari kwa mazungumzo.

Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amesema muda umewadia wa kufanya mazungumzo ya kutafuta amani na kuzitaka pande zinazozana kukutana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Martin Griffiths nchini Sweden mwezi ujao ili kufikia suluhisho.

Je, mapigano yatatulia Yemen?

Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ametaka mashambulizi yote ya angani yanayofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kusitishwa mara moja katika maeneo yaliyo na makazi ya raia.

Singapur Jim Mattis IISS Shangri-la Dialog
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim MattisPicha: Getty Images/AFP/R. Rahman

Aidha amewataka waasi wa Houthi kukoma kurusha makombora na kufanya mashambulizi kwa kutumia ndege zisizoendeshwa na marubani dhidi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Zaidi ya watu 10,000 wameuawa katika mzozo huo wa Yemen na zaidi ya watu milioni 22 ambayo ni theluthi mbili ya idadi jumla ya Wayemeni wakihitaji misaada ya kibinadamu na wengine milioni 8.4 wako katika hatari ya kufa njaa.

Yemen ni moja ya mataifa masikini zaidi ya kiarabu na limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka minne iliyopita.

Mahusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia yamepooza katika wiki za hivi karibuni kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa mrithi wa kiti cha mfalme Mohamed bin Salman.

Saudi Arabia na washirika wake waliingilia kati mzozo wa Yemen mwaka 2015 kumuunga mkono Rais Abedrabbo Mansour Hadi anayepambana dhidi ya waasi wa Houthi. Muungano huo umesema umetuma majeshi katika pwani ya Hodeida kabla ya operesheni ya kijeshi dhidi ya Wahouthi inayotarajiwa kuanza siku chache zijazo.

Marekani imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kuunga mkono muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudia hasa baada ya mashambulizi kadhaa ya angani kuwalenga raia.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga