Mashambulizi ya kigaidi na hotuba ya Steinemeier Magazetini
5 Aprili 2017Tunaanzia kaskazini magharibi mwa Syria ambako jumuia ya kimataifa inaionyeshea kidole serikali ya Rais Bashar Al Assad kuwa nyuma ya mashambulizi ya kemikali yaliyoangamiza maisha ya zaidi ya watu 100 wakiwemo watoto. Gazeti la "Rhein-Neckar Zeitung" linaandika: "Kwa mara nyengine tena, kimedhihirika kile ambacho tokea hapo kilikuwa dhahir: Ufumbuzi wa kudumu wa kisiasa ni muhali kufikiwa pamoja na Bashar al Assad. Vipi wasyria wanaweza kumkubali kiongozi wa serikali anaewashambulia wananchi wake kwa mabomu ya kemikali. Na vipi kiongozi kama huyo anaechukiwa kupita kiasi anaweza kuleta utulivu nchini mwake, kama wananchi tangu awali wamekuwa wakiteremka majiani dhidi yake? Hata hivyo Assad ana kinachomzuzuwa. Anajivunia uungaji mkono usiokuwa na masharti wa Vladimir Putin; Umoja wa Mataifa hauna lake mbele ya kura ya turufu ya Urusi-hali inayolizusha upya suala kama mfumo wa madola matano yenye haki ya kutumia kura ya turufu na kuzuwia kila azimio la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, unalingana na wakati.
Kitisho cha mashambulizi ya kigaidi Urusi
Nchini Urusi pia maisha ya binaadam yameangamia. Shambulio la kigaidi limepelekea watu wasiopungua 14 kuuwawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa mjini St.Petersburg. "Urusi yazongwa upya na mashambulizi ya kigaidi" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Thüringische Landeszeitung",linaloendelea kuandika: "Kimoja ni dhahir baada ya kuripuliwa mabomu St.Petersburg: Uwanja wa mashambulizi nchini Urusi ni mpana. Hatari itakuwa kubwa zaidi pindi maelfu ya wapiganaji wa dola la kiislam IS wakirejea katika eneo la kaskazini mwa Caucasus. Hakuna sababu ya kushangiria hata kama siasa za Putin zinakosolewa. Tangu mwaka 2015, miji ya Paris, Brussels, Nice, Berlin, London na sasa St.Petersburg imeshambuliwa. Kesho itakuwa pengine miji ya Roma, Warsaw au Munich itakayohujumiwa. Mapambano dhidi ya ugaidi yatadumu miaka. Hata hivyo dawa ni moja tu: ushirikiano wa dhati wa kimataifa, kubadilishana habari kati ya idara za upelelezi na kuimarisha mitambo ya digitali dhidi ya vyenzo vya propaganda za wanajihadi.
Steinmeier ashadidia umuhimu wa Ulaya mjini Strassburg
Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amelitembelea bunge la Umoja wa Ulaya na kuhutubia. Hakuficha msimamo wake, linaandika gazeti la "Schwebische Zeitung": Steinmeier amezungumzia kuhusu jukumu la uongozi mjini Strassburg na kusema jukumu hilo linabebwa na wote barani Ulaya, lakini Ujerumani pengine ingebidi iwajibike zaidi kidogo kuliko wengine. Steinemeier amechukua msimamo, kuelekea Ulaya.Yabainika kuanzia sasa atakuwa akiutumia wadhifa wake kutathmini zaidi yanayojiri katika nyanja za kisiasa kuliko alivyokuwa akifanya mtangulizi wake. Na hivyo ni sawa kabisa. Nani kama si Steinemeier, anaebidi kuwapa watu moyo kuhusu umuhimu wa muungano wa Ulaya? Steinemeier anatokana na kizazi kilichokulia katika vuguvugu la Ulaya.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef