Mataifa ya kigeni yawajongelea watawala wapya wa Syria
16 Desemba 2024Hayo yanatokea ikiwa ni wiki moja baada ya waasi wenye misimamo ya kiislamu kuuangusha utawala wa Rais Bashar al-Assad.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Geir Pedersen, ni miongoni mwa wanadiplomasia walioutembelea mji mkuu wa Syria, Damascus ambako alikutana na kiongozi wa waasi Abu Mohammedi al-Jolani.
Mwadiplomasia huyo alitoa mwito wa "haki na uwajibikaji kwa uhalifu uliofanywa" na kuwarai watawala wapya kuhakikisha wanatumia mifumo rasmi ya utoaji haki bila kufanya vitendo vya kulipa kisasi.
Ujumbe wa Qatar nao uliwasili jana mjini Damuscus ukiahidi kuwaunga mkono kikamilifu watu wa Syria kufuatia kile ujumbe huo umekiita "mafanikio ya mapinduzi ya umma". Ufaransa nayo inapanga kutuma ujumbe wake kesho jumanne kuitembelea Syria.
Mataifa kadhaa ya kiarabu yamefungua shughuli tena ofisi zao za ubalozi huku Uingereza na Marekani zikithibitisha kufanya mazungumzo ya moja kwa mmoja na waasi wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham lililoupindua utawala wa Assad.