1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mazishi ya waziri mkuu wa zamani wa India Singh yaanza

28 Desemba 2024

Mazishi ya kitaifa ya Manmohan Singh, waziri mkuu wa zamani wa India anayetazamwa sana kama ndiye aliyebuni wa mpango wa mageuzi ya uchumi wa nchi, yameanza rasmi leo hii huku wanasiasa na umma ukiomboleza kifo chake.

https://p.dw.com/p/4odsT
Indien Neu Delhi Trauerzug  Manmohan Singh
Maafisa wa usalama na wengine wakitembea na gari la kubebea maiti lililobeba mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa India Manmohan Singh kuelekea mahali pa kuchomwa maiti huko New Delhi, India, Jumamosi, Desemba 28, 2024.Picha: AP Photo/picture alliance

Asubuhi hii mwili wake ulipelekwa katika ofisi za makao makuu ya chama chake cha  Congress mjini New Delhi, ambapo viongozi wa chama na wanaharakati walitoa heshima zao kwake huku wakiimba "Manmohan Singh ataishi milele." Baadaye, mwili wa Singh ulisafirishwa hadi mahali pa kuchomea maiti kwa ajili ya ibada za mwisho. Mamlaka ilitangaza kipindi cha siku saba za maombolezo na kuzuia matukio yoyote ya kitamaduni na burudani katika kipindi hicho. Kiongozi huyo mkongwe, ambaye pia alipewa sifa kwa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia na Marekani, alifariki dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 92.