Mazoezi ya kijeshi dhidi ya ugaidi kuanza karibuni
20 Agosti 2016Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la "Rheinische Post " toleo lake la Jumamosi (20.08.2016) Klaus Bouillon mkuu wa mawaziri wa mambo ya ndani wa majimbo nchini Ujerumani amesema mazoezi hayo ya kupambana na ugaidi ya jeshi la Ujerumani Bundeswher yanaweza kuidhinishwa mwishoni mwa mwezi huu.
Bouillon ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la magharibi la Saarland ameliambia gazeti hilo "Nataraji kwamba waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen na waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere wataidhinisha mazoezi hayo hapo tarehe 31 mwezi wa Augusti."
Amesema pia kwamba anaona kuna harakati fulani katika majimbo yanayoongozwa na chama cha SPD kuridhia kuwepo kwa ushirikiano kati ya Bundeswehr na polisi wakati wa matukio ya kigaidi na majanga mengine.
Mazoezi taifa zima
Waziri wa mambo ya ndani wa Lower Saxony Boris Pistorius imeripotiwa kwamba amependekeza katika baruwa aliyomtumia Boillon kwamba majimbo yote 16 ya Ujerumani yanapaswa kufanya mazoezi hayo ya pamoja ya kupambana na ugaidi kati ya jeshi na polisi.
Kwa mujibu wa gazeti la "Redaktionszwerk Deutschland" lililokariri baruwa hiyo Postorius alipendekeza kwamba mazoezi hayo yafanyike nchini nzima kwa mujibu wa sheria na chini ya uongozi wa polisi.
Katiba ya Ujerumani kutokana na kutumiwa vibaya kwa jeshi kudhamini ugaidi wa taifa wakati wa utawala wa enzi ya Manazi, inaruhusu tu kutumika kwa jeshi chini ya mazingira maalum na tishio la uhakika kutoka nje.Hapo mwaka 2012 hukumu ya Mahakama ya Katiba iliamuwa kwamba Bundeswher linaweza pia kutumiwa wakati wa mashambulizi ya kigaidi.
Mkakati mpya wa kijeshi
Mwezi wa Julai wizara ya ulinzi ilithibitisha mazingira hayo ya kisheria katika waraka wake wa serikali wenye kuainisha mkakati wa kijeshi wa Ujerumani.
Mazoezi hayo yatakuwa ushirikiano wa kwanza kati ya polisi na jeshi kujiandaa na mashambulizi ya kigaidi.
Kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi nchini Ujerumani baadhi yao Dola la Kiislamu likidai kuwa na mkono wake, Kansela Angela Merkel ametowa wito wa kutumika kwa jeshi ndani ya nchi iwapo kutatokea kitendo kikubwa cha ugaidi.
Kipengele cha nne kati ya tisa viliomo katika mpango uliowasilishwa na Merkel kupambana na ugaidi unaoweza kutokea nchini kinasema kwamba Ujerumani imevuka kizingiti cha kisaikolojia. Merkel amesema kuanzia sasa jeshi la Ujerumani litafanya kazi ndani ya ardhi ya Ujerumani kwa kushirikiana na polisi pindipo kutatokea shambulio kubwa la kigaidi.
Kumewahi kuwepo kwa mazoezi ya pamoja kati ya jeshi na polisi hapo kabla mfano operesheni ya LÜKEX imeanzishwa ili kukabiliana na mafuriko katika mwambao wa kaskazini nchini Ujerumani lakini hii ni operesheni ya kwanza kwa ajili ya ugaidi.
Serikali inakiri kwamba hiyo ni changamoto kubwa kuwakusanya pamoja wahusika tafauti na kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua yenye ufanisi ilioratibiwa kwa pamoja.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ AP/dpa
Mhariri : Isaac Gamba