Merkel ahangaika kutafutia ufumbuzi suala la wahamiaji
22 Juni 2018Kansela Angela Merkel amekutana na Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri, katika ziara yake ya siku mbili ambapo pia anatarajiwa kukutana na maafisa, wafanyabiashara na wajumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa. Merkel aliwasili Beirut jana akitokea Jordan ambayo pia ni jirani ya nchi inayokabiliwa na vita ya Syria. Ziara hii katika eneo hilo la Mashariki ya Kati inafanyika wakati nyumbani Ujerumani, Merkel mwenyewe anakabiliwa na mgogoro kuhusu suala la wahamiaji. Zaidi ya Wasyria milioni 6 wamekimbia vita na kuingia katika nchi za Jordan, Lebanon na Uturuki na maelfu ya wengine wamekimbilia Ulaya kupitia Bahari ya Medittereania.
Kansela Merkel yuko mjini Beirut nchini Lebanon hivi sasa, nchi ambayo imepokea maelfu kwa maelfu ya watu waliokimbia vita nchini Syria. Maafisa wa Lebanon wanasema uchumi wa nchi yao unaporomoka na wanawatolea mwito Wasyria warudi nyumbani katika maeneo ambayo yana utulivu kiasi. Nchi za kanda hiyo zinasema hazipokei msaada wa kutosha wa kimataifa kwa kupokea mzigo mkubwa wa wakimbizi kutoka Syria.
Kansela Merkel anafanya mazungumzo leo na Waziri Mkuu Saad Hariri na kikubwa kinachotegemewa kugubika mazungumzo yao ni suala la wakimbizi na uhamiaji. Lebanon inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na hata kushindwa kuendesha huduma za msingi kwa wananchi wake kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi.
Merkel anatembelea shule inayoendeshwa kawaida mjini Beirut kujionea wanafunzi 600 wanavyofundishwa madarasani na baadaye kukaa na Waziri Mkuu Hariri kwa mazungumzo ya kina kabla ya kuzungumza mbele ya waandishi habari mchana huu.
Serikali ya Ujerumani inatarajia kwamba kwa kutoa msaada kwa majirani wa Syria katika hatua ya kuunga mkono juhudi zao za kuwapokea wakimbizi wa Kisyria inaweza ikapunguza wimbi la wahamiaji wanaokimbilia Ujerumani.
Kansela huyo wa Ujerumani anakabiliwa na mvutano mkubwa nyumbani kwake kuhusu wakimbizi akilumbana na waziri wake wa mambo ya ndani, Horst Seehofer, anayetishia kuifunga mipaka ya nchi hiyo ikiwa Kansela atashindwa katika mpango wake wa kutafuta suluhisho na nchi za Ulaya, Mashariki ya Kati na washirika wake wa Afrika ya Kaskazini ili kuhakikisha idadi ya wahamiaji inapungua. Akizungumza Jordan (21.06.2018) Merkel aligusia juu ya mgogoro huo wa wakimbizi kwa kusema:
''Naamini mnachohitaji kwa ujumla sio kuwa na hofu.Ni wazi siwezi kuacha kusema kwamba wakati mwingine tunao watu wanaoweza kutoa kauli za kutia hofu,lakini nafikiri kwamba hilo linaweza kutokea kokote. Lakini kwa ujumla naweza kusema Ujerumani bado ni nchi salama japo yamekuwepo matukio ambapo raia wakigeni wamekuwa wakituhuimiwa na kushambuliwa,lakini kwa bahati mbaya ni kwamba pia yamekuwepo matukio ambapo kwa mfano wakimbizi wameua wasichana wadogo.Kwahivyo matukio kama hayo yapo pande zote.''
Merkel ameiahidi Jordan dola milioni 100 za kusaidia utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi.
Hata hivyo leo(22.06.2018) chama cha Christian Social Union cha waziri wa ndani anayetafautiana na Merkel kinasema mpango wa kansela wa kuzijumuisha nchi nyingine za Umoja wa Ulaya katika kutafuta suluhu la tatizo na uhamiaji haupaswi kufanyika kwa gharama za walipa kodi wa Ujerimani.
Merkus Ferber mwanachama wa ngaziya juu katika chama hicho ndugu na CDU anasema wanawasiwasi kwamba Merkel ataanza kuzunguka Ulaya na kitabu cha hundi kuziahidi nchi hizo za ulaya. Wiki hii Merkel alisema atatoa msaada kwa nchi ambazo zitakubali kuwachukua wahamiaji waliokataliwa Ujerumani katika mpango sawa na ule uliofikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki.
Merkel amepanga mkutano mdogo Jumapili na nchi za Ulaya kujaribu kutafuta suluhu lakini baadhi ya nchi hizo kama Poland, Jamhuri ya Czech, Slovakia na Hungary zimeshathibitisha kwamba hazitokanyaga kwenye mkutano huo zikisema kwamba hazimo kwenye kundi la wapenda wahamiaji. Italia ambayo pia ilitarajiwa ihudhurie mkutano wa Merkel waziri mkuu wake Giuseppe Conte amesema wamejiondoa baada ya kulumbana na Merkel kuhusu suala hilo lililoigawa vipande Jumuiya hiyo ya Ulaya.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef