1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ataka wakimbizi waajiriwe Ujerumani

Admin.WagnerD15 Septemba 2016

Kansela wa Ujeruamni Angela Merkel amesema Ujerumani inahitaji suluhisho madhubuti kuwajumuisha wakimbizi katika soko la ajira la Ujerumani kama nguvu kazi. Merkel aliyasema hayo baada ya kukutana na kampuni mbalimbali.

https://p.dw.com/p/1K2yY
Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Katika juhudi za kuyatetea maisha yake katika siasa, Bi Merkel aliwaita wakuu wa baadhi ya kampuni kubwa kabisa za Ujerumani kwa ajili ya mkutano mjini Frankfurt kufafanua kwa nini hawajachukua hatua kuwapa ajira wakimbizi na pia kubadilishana mawazo kuhusu jinsi wanavyoweza kushirikiana.

Kampuni nyingi zinahoji kwamba ukosefu wa ujuzi wa lugha ya Kijerumani, wakimbizi wengi kushindwa kuthibitisha wana sifa au vigezo na pia kukosekana uhakika wa wao kuendelee kuishi Ujerumani, ina maana hakuna mengi ambayo kampuni hizo zinaweza kuyafanya katika kipindi kifupi.

Kansela Merkel ameiambia radio ya rbb-inforadio kwamba ikihitajika, mazingira maalumu yanaweza yakaandaliwa kuharakisha mchakato wa kuwajumuisha wakimbizi katika soko la ajira, lakini akakiri hilo pia litachukua muda.

Utafiti uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kampuni 30 zinazowakilishwa katika soko la hisa la Ujerumani, DAX, wiki iliyopita, umebaini kuwa ziliwaajiri jumla ya wakimbizi 63. Hamsini kati yao wameajiriwa na kampuni ya Deutsche Post DHL, ambayo imesema iliwapa ajira wakimbizi kupanga na kusambaza barua na vifurushi. Mkuu wa kampuni ya DHL, Frank Appel, alisema jana kuwa kampuni hiyo sasa imewaajiri wakimbizi zaidi, hadi kufikia jumla ya 102.

Deutschland Flüchtling Hamza Ahmed in der Firma Reuther STC GmbH in Fürstenwalde
Mkimbizi Hamza Ahmed katika kampuni ya Reuther STC GmbH mjini Fürstenwalde, UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/P. Pleul

Mkurugenzi wa kampuni ya viwanda ya Ujerumani ya Thyssenkrupp, Heinrich Hiesinger, alidokeza mapema mwezi huu kwamba kuwaajiri wakimbizi sio suluhisho la uhaba wa ujuzi na nguvu kazi nchini.

Kampuni nyingi za Ujerumani, hasa za uzalishaji bidhaa, hupendelea kuwaajiri wafanyakazi kupitia mipango ya kuwafunza kazi iliyoratibiwa, ambapo huwafunza vijana kwa muda wa hadi miaka minne kwa ajira zinazohitaji ujuzi wa hali ya juu, na wakati mwingine kazi maalumu za kampuni. Lakini kampuni zinasema wakimbizi wengi waliowasili kutoka Syria, Iraq, Afghanistan na kwingineko, kwa kiwango kikubwa hawajajiandaa kwa mafunzo ya aina hiyo.

Vurugu eneo la Mashariki

Wakati haya yakiarifiwa polisi wamevunja makabiliano makali kati ya wajerumani wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia na wahamiaji wanaotafuta vibali usiku wa kuamkia leo katika mji wa mashariki wa Bautzen.

Msemaji wa polisi Thomas Knaup, amesema wanaume na wanawake 80 na wahamiaji wapatao 20 walikabiliana katika uwanja ulio katikati ya mji huo jana usiku. Knaup aidha amesema baadhi ya wahamiaji waliwarushia chupa na vitu vingine maafisa wa polisi ambao waliwakabili kwa virungu na kuweka uzio kuyatenganisha makundi hayo mawili. Tukio hilo linaashiria ongezeko la hali ya wasiwasi nchini Ujerumani kuhusiana na sera ya wakimbizi ya kansela Merkel.

Deutschland Bautzen Konflikt Flüchtlinge vs Rechte
Machafuko ya mjini BautzenPicha: picture-alliance/dpa/Xcitepress

Mkazi mmoja mwenye umri wa miaka 18 alihitaji matibabu hospitalini kufuatia majeruhi ya kukatwa usoni aliyoyapata, polisi wamesema. Wakati gari ya kubebea wagonjwa ilipowasili katika eneo la tukio, ilishambuliwa kwa mawe na watu wenye misimamo mikali. Ilibidi gari la pili liagizwe ili raia huyo wa Morocco apelekwe hospitali.

Mji wa Bautzen umekabiliwa na maandamano ya Wajerumani wenye misimamo mikali dhidi ya wakimbizi katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi Februari watu wa kundi lenye msimamo mkali walishangilia wakati makazi ya wakimbizi yalipokuwa yakiungua katika mji huo na kuwazuia maafisa wa zima moto kuuzima moto huo.

Upinzani wa sera ya kansela Merkel ya kuwakaribisha wakimbizi umefikia kiwango cha juu kabisa Ujerumani, ambayo iliwachukua wahamiaji wapatao milioni 1.1 mwaka 2015.

Mwandishi:Josephat Charo/dpae/rtre

Mhariri:Daniel Gakuba