1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aunga mkono amani ya Israel na Palestina

24 Machi 2017

Merkel asema haoni njia mbadala ya kupatikana amani kwa njia nyingine isipokuwa kwa kuundwa madola mawili yatakayoishi kwa amani

https://p.dw.com/p/2ZuQN
Berlin Mahmud Abbas bei Merkel
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Kansela Angela Merkel amethibitisha kwa mara nyingine leo juu ya msimamo wa Ujerumani wa kuunga mkono amani ya mashariki ya kati kwa kupatikana suluhu ya kuundwa madola mawili. Merkel amesisitiza kwamba haoni njia nyingine mbadala ya kutafuta amani zaidi ya kupatikana suluhu ya madola mawili.Kauli ya Merkel imeongeza matumaini kwa Wapalestina kwamba kansela huyo atakuwa msuluhishi katika kufikiwa makubaliano ya amani ya hapo baadae.

Wakizungumza kwa pamoja na waandishi wa habari Kansela Merkel na rais wa mamlaka ya Wapalestina wameonekana kuelewana kuhusu masuala waliyojadliana katika mkutano wao uliofanyika leo.Kansela Merkel amesema kwamba hajaona njia nyingine mbadala zaidi ya mpango wa kuundwa madola mawili katika kupatikana amani ya mashariki ya kati.

''Nataka kuweka wazi msimamo wa Ujerumani kuhusu suluhisho litakalopatikana kwa kuundwa madola mawili.Tunahitaji uthabiti katika kuendeleza mpango huo wa kupatikana suluhu ya kuundwa madola mawili.Kama ilivyokuwa mwanzo sioni kitu kingine mbadala zaidi ya mpango huo wa madola mawili.Wapalestina na waisrael wana haki ya kuishi kwa usalama na amani na hakuna njia nyingine ya kuhakikisha hilo isipokuwa kupitia mpango huo.Na licha ya kwamba ni mpango unaokabiliwa na changamoto tunapaswa kuendelea kujaribu kuutimiza mpango huo''

Msimamo huo wa Ujerumani umekuja wakati ambapo wapalestina wameghabishwa kutokana na hatua ya katikati ya mwezi Februari ya rais wa Marekani Donald Trump kuufuta  utaratibu uliokuwa unafuatwa na nchi hiyo ya Marekani kwa miongo kadhaa wa kuunga mkono mpango wa kupatikana suluhisho la mashariki ya kati kwa kuundwa madola mawili yatakayoishi bega kwa bega kwa aman.Trump alisema kwamba utawala wake utaunga mkono makubaliano ya aina yoyote  yatakayoziridhisha pande zote mbili Palestina na Israel.Hata hivyo leo hii Kiongozi wa mamlaka ya Wapestina Mahmoud Abbas mjini Berlin ameishukuru serikali ya Kansela Angela Merkel kwa kuinga mkono Palestina kwa hali na mali na zaidi kuitaka Ujerumani kubeba dhima kubwa katika kuumaliza mgogoro kati ya Wapalestina na Waisrael mgogoro uliodumu miongo kadhaa.

USA Donald Kampagne Rede in Louisville
Picha: Reuters/J. Sommers

''Mpendwa Kansela Merkel tutazingatia mpango mbadala wa  kuundwa madola mawili ili kufikia amani ya dhati ya kudumu.Hii ina maana tunabidi kuwafanya Waisraeli wafikishe mwisho hatua ya kuikalia ardhi ya wapalestina.Na bila shaka masuali yote kuhusu hadhi yetu yanabidi kubainishwa ili kufikiwa makubaliano ya amani ya kudumu.Na hii ndio njia pekee ya kufikia amani ya kudumu ili watu wa Israel na Palestina waweze kusihi kwa usalama na kukubaliana kuhusu mipaka ya ndani''

Wadadisi wengi katika mashariki ya kati wanahisi kwamba suala la kufikiwa suluhu ya kuundwa madola mawili lina nafasi ndogo ya kufanikiwa na hasa kwakuwa Israel wakati huu imekuwa ikiendeleza ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi na kwa upande mwingine Wapalestina wenye msimamo mkali wamekuwa wakiishambulia Israel kwa mabomu mara kwa mara.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri Iddi Ssessanga

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW