Merkel : Makosa yalifanyika katika suala la wakimbizi
31 Agosti 2016Merkel alisema kwamba ni wazi kabisa Ujerumani ni nchi madhubuti na dhamira yeo inapaswa kuwa tayari wameweza kumudu mambo mengi kwa hiyo wanaweza kumudu suala la wakimbizi na iwapo watakuwa na vizingiti njiani hawana budi kuvishinda na nchi itafanya kila iwezalo kwa kushirikiana na serikali za majimbo kufanikisha jambo hilo.
Ilikuwa ni tarehe 31 mwezi wa Augusti mwaka 2015 wakati Kansela Angela alipotowa kauli yake hiyo mashuhuri "wir schaffen das" tutalimudu hili wakati Ujerumani ilipowakaribisha mamia kwa maelfu ya wakimbizi na wahamiaji nchini waliokuwa wakikimbia vita na mizozo nchini mwao.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung yaliyochapishwa leo juu ya kauli mbiu yake hiyo ambayo imewagawa wananchi wa Ujerumani kimtizamo Merkel amesisitiza kwamba inaendelea kubakia kiini sahihi kwa jukumu la kukabiliana na mzozo huo.
Kansela Merkel ambaye kwa miezi kadhaa alikabiliwa na shutuma kwa kuonyesha moyo huo wa kujiamini kwa matumaini katika kuwashughulikia wakimbizi ameliambia gazeti hilo la Ujerumani kwamba Ujerumani na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yalishindwa kuchukuwa hatua licha ya kuwepo kwa ushahidi ya mzozo huo kuzidi kuwa mkubwa.
Makosa yamefanyika
Merkerl amesema kuna masuala ya kisiasa ambayo mtu anaweza kuyaona kuwa yanakuja lakini kwa wakati fulani hayawaingii watu akilini na nchini Ujerumani wamelipuuza tatizo hilo kwa muda mrefu halikadhalika kuzuwiya hata na haja ya kutafutafuta usuluhishi wa umajumui wa Ulaya. Ameongeza kusema kwamba Ujerumani kwa miaka kadhaa imekuwa pia ikifanya makosa kwa kupinga mpango wa kugawana wakimbizi kwa uwiano na kulitupia jukumu hilo idara ya mipaka ya majini ya Umoja wa Ulaya.
Merkel amesema wakimbizi wengi walikuja mwaka 2004 na mwaka 2005 na wakaiwachilia Uhispania na wengine wa Idara ya Umoja wa Ulaya ya masuala ya mipaka ya nje kuwashughulikia. Amesema Ujerumani ilikuwa na furaha sana kwamba baada ya kupokea wakimbizi wengi wakati wa vita nchini Yugoslavia nchi nyengine sasa zilikuwa zinastahiki kulishughulikia suala hilo amesema jambo hilo hawezi kulikanusha.
Katika mahojiano hayo Merkel pia amekaririwa akisema "Ujerumani itabakia kuwa Ujerumani ikiwa na kila kitu ambacho inakipenda "
Ameongeza kusema mabadiliko yamekuwa yakitokea kwa miongo mingi lakini mabadiliko sio kitu kibaya yanahitajika katika maisha jambo lililo wazi ni kwamba Ujerumani haitoyaacha maadili yake.
Ugaidi hauletwi na wakimbizi
Kansela Merkel pia ameyatumia mahojiano hayo kuwashutumu wanasiasa wa Ujerumani kwa kuwataka wasitumie lugha kali na wasishiriki kupalilia kauli kwamba vitisho vinatoka nje.
Merkel ni "wazi sio sahihi kwamba ugaidi unaletwa na wakimbizi " na kwamba " tayari ulikuwepo hapa katika aina mbali mbali na kwamba wanaotaka kufanya mashambulizi wamekuwa wakisubiri kufanya hivyo."
Merkel na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya wameshindwa kupiga hatua kubwa katika juhudi za kuyashirikisha mataiafa mengine ya Umoja wa Ulaya kugawana mzigo wa wakimbizi wanaowasili hivi sasa.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters,AFP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga