Miaka 57 ya shirika la afya la kimataifa WHO
7 Aprili 2005:
Shirika la Afya la umoja wa mataifa,WHO,limeundwa april sabaa mwaka 1948 na kulingana na muongozo wake,lengo ni kuhakikisha hali nzuri ya afya kwa binaadam wote ulimwenguni.Katika muongozo wa shirika la WHO,afya inatajwa kua ni hali nzuri kimwili,kiakili na kijamii na sio tuu ukosefu wa maradhi au udhaifu.Lakini bado ni wachache kabisa ndio wanaojivunia afya kama sehemu kamili ya haki ya binaadam.Tarakimu zinaonyesha kila dakika moja anafariki mama mmoja kutokana na shida anapokua mjamzito au anapotaka kujifungua ,shida ambazo zinaweza kuepukwa.Hali hii inadhihirisha wazi jinsi mwanamke anavyonyanyaswa katika jamii.Na inazidisha pia hisia ya unyonge na dhulma.
Pengine inaingia akilini unapowaaona wazee kwa mfano wale wa Terri Schiavo,wakipigana kufa kupona kutaka binti yao aendelee kutibiwa.Thamani ya maisha ya kiumbe katika nchi za magharibi ni ya juu na vyombo vya habari navyo huzidi pia kuwatanabahisha walimwengu linapohusika suala la maadili la uhai au kifo.
Lakini hakuna ,si bunge,si serikali na wala si kiongozi wa serikali anaeitisha kikao cha dharura au kupitisha maamuzi linapohusika suala la mama na mtoto ambao kitisho chao kikubwa kinaanzia wakati wa kujifungua.
Hakuna sheria inayomlinda mama na mtoto katika nchi masikini kabisa za dunia,ili kuhakikisha maisha yao yananusurika.
Na kusema kweli masaibu hayo sio kwamba hayawezi kuepukwa,hasha:Kila mwaka watoto milioni tatu wanazaliwa maiti na vijana zaidi ya milioni 10,wake kwa waume wanakufa hata kabla ya kufika umri wa miaka mitano.Jambo dogo tuu,mfano chandarua, maelezo,usafi majaumbani ,maji safi au hata huduma za kawaida za afya,lingeweza kuyanusuru maisha ya watoto kadhaa.Na sio tuu wao peke yao,hata mama zao wangeweza kufaidika pindi serikali zingewajibika ipasavyo.Kwa mfano wanawake wangeruhusiwa kufuata mpango wa uzazi wa majira,basi idadi ya wakinamama wanaokufa kwa mwaka wakati wakiwa wajawazito au wanapokua wanajifungua ingepungua angalao kwa thuluthi moja.
Ikiwa katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara,mwanamke mmoja kati ya 16 anakufa kwasababu ya shida zinazozababishwa na mimba au wakati wa kujifungua-basi hilo haliwezi kutajwa kua ni balaa na msiba tuu bali pia uzembe na mapuuza katika kuthamini maisha ya binaadam.
Pale wakfu wa Ujerumani unapolalamika , jumuia ya kimataifa haitekelezi ahadi ilizotoa wakati wa mkutano wa kimataifa wa idadi ya wakaazi wa dunia,mjini Cairo mwaka 1994,basi,lawama hizo hazimaanishi pekee kua malengo ya millenium yaliyowekwa na umoja wa mataifa hayataweza kufikiwa,bali pia lawama hizo ni kilio dhidi ya kuzuwiliwa kutolewa misaada.
Na ikiwa kwa mfano shirika la misaada la Ujerumani-Madaktari wasiojali mipaka linalalamika huduma za madawa kwaajili ya watoto walioambukizwa vijidudu vya maradhi ya ukimwi ni haba mno katika nchi za ulimwengu watatu,basi lawama hizo sio tuu kwasababu ya ukosefu wa soko ya kuvutia viwanda vya madawa kuweza kutengeneza tiba kwaajili ya watoto bali hasa kwasababu ya kutenganishwa suala la afya na suala zima la haki za binaadam.
Bila ya afya,hakuna chochote kinachowezekana,na ili iweze kubakia kua nzuri,watu wa nchi za viwanda za magharibi wanatoa fedha chungu nzima kugharimia miradi ya afya na zana za matibabu .Hiyo ni sawa kabisa.Lakini kuwanyima mama na watoto katika nchi masikini za duni,huduma za kimsingi za afya si ubinaadam si haki na ni jambo la hatari pia .Kwasababu yeyote yule anaejihisi jumuia ya kimataifa haimthamini,haitamuia vigumu nae pia kutouthamini ulimwengu.Lakini hatima yetu iko katika ulimwengu huo huo ambako haki za kiumbe kuwa na afya nzuri zinaendelezwa kwa hawa na kwa wengine zinageuka ukweli wa mambo.