1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogherini aionya Marekani kutoingilia siasa za Ulaya

11 Februari 2017

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini aitahadharisha Marekani dhidi ya kuingilia shughuli za kisiasa barani Ulaya baada ya maafisa wa Marekani kutaka kujuwa taifa gani litajitowa baada ya Uingereza.

https://p.dw.com/p/2XOkq
Brüssel Brexit Gipfel Federica Mogherini
Picha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Mogherini amekaririwa akisema baada ya kukamilisha mikutano yake na maafisa wa serikali ya Marekani akiwemo waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson kwamba "Hatuingilii siasa za Marekani na watu wa Ulaya wanategemea Marekani haitoingilia siasa za Ulaya."

Mwaka jana Trump alipongeza uamuzi wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni inayotajwa kama "Brexit" na kuzusha wasi wasi katika umoja huo wote kwamba yumkini akataka kuyumbisha mradi wa muungano wa umoja huo wa Ulaya.

Mogherini amesema "Naamini umoja wa Umoja wa Ulaya hivi leo unajidhihirisha zaidi kuliko ilivyokuwa miezi michache iliopita."

Amesema Uingereza itaendelea kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya kwa angalau kwa miaka mengine miwili  na haitoweza kuzungumzia makubaliano yoyote ya biashara peke yake na nchi yoyote ya tatu hadi hapo itakapokuwa imeondoka Umoja wa Ulaya.

Kuhujumu Umoja wa Ulaya ni wenda wazimu

Belgium | Der amerikanische Botschafter bei der EU Anthony Gardner
Aliyekuwa balozi wa Marekani kwa Umoja wa Ulaya Anthony Gardner. Picha: picture-alliance/W. Dabkowski

Tokea ushindi wake katika uchaguzi wa mwezi wa Novemba viongozi kadhaa wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamemkosowa Trump kutokana na kauli zake za kugawa watu huku Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akisema "Sisi nwananchi wa Ulaya hatima yetu iko mikononi mwetu."

Mogherini amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Tillerson pamoja na maafisa wengine wa serikali ya Marekani mjini Washington.

Wakati huo huo Mogherini ametaja kwamba Ikulu ya Marekani bado haikumchaguwa balozi wa Marekani kwa Umoja wa Ulaya ambayo ina nchi wanachama 28 ambazo itabidi zimridhie katika utaratibu uliokuwa ukitumika kwa muda mrefu.Wanasiasa wameelezea kutofurahishwa kwao juu ya uwezekano wa kuteuliwa kwa Theodore Roosevelt Malloch kushika wadhifa huo.

Kabla ya kuondoka kwenye wadhifa wake mwezi wa Januari balozi wa zamani wa Marekani kwa Umoja wa Ulaya Anthony Gardner aliuonya utawala wa Trump kutounga mkono kuvunjika kwa umoja huo.

Gardner aliyeteuliwa na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amesema timu ya mpito ya Trump imewasiliana na maafisa kadhaa wa Umoja wa Ulaya kabla ya kuapishwa kwa Trump na kuwauliza nchi gani yumkini ikajitowa kwenye umoja huo baada ya Uingereza.

Gardner amesema katika mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari  "kufikiri kuunga mkono kumegeuka kwa Ulaya tutatukuwa tunaendeleza maslahi yetu utakuwa ni upuuzi mtupu.Ni wenda wazimu".

Kauli za Trump zazusha mashaka

Washington Rex Tillerson empfängt  Federica Mogherini
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson mjini Washington.Picha: picture alliance/AP Images/A. Harnik

Wakati wa kampeni yake Trump aliapa kuutupilia mbali mkataba wa Iran iliofikia na mataifa yenye nguvu duniani hapo mwaka 2015 na kudhibiti ipasavyo mpango wa nyuklia wa nchi hiyo ili nchi hiyo iondolewe vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa.

Suala la kunusurika kwa mkataba huo liko wazi itategemea  iwapo utawala wa Trump utajitowa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa. Hata hivyo mwanasiasa huyo mwandamizin wa Umoja wa Ulaya amesema Ikulu ya Marekani imemhakikishia kwamba mkataba huo utabakia kama ulivyo.

Mogherini amewaambia waandishi wa habari hapo Ijumaa amehakikishiwa kwa kile alichokisikia katika mikutano hiyo juu ya nia ya kuendelea kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo.

Mogherini amesema jukumu lake kubwa wakati wa ziara yake hiyo mjini Washington ilikuwa ni kuhakikisha kwamba mkataba wa Iran unanusurika katika utawala wa Trump.

Mohamed Dahman/Reuters/AFP/EFE

Mhariri : John Juma