Mshukiwa shambulizi la Magdeburg alitoa vitisho mara mbili
31 Desemba 2024Wizara ya Sheria katika jimbo la kaskazini mashariki la Mecklenburg-Vorpommern imesema mshukiwa huyo aliyetambuliwa kwa jina Taleb A aliashiria kuwa angefanya vitendo vya mashambulizi mara mbili kabla ya shambulio hilo la Desemba 20, ambalo liliwauwa watu watano na kuwajeruhi wengine zaidi ya 230.
Mnamo Aprili 2013, daktari huyo ambaye alikuwa amekasirishwa na kile alichoona kuwa ni kucheleweshwa kwa mtihani wake wa kitalaamu, alimtishia kwenye simu mfanyakazi mmoja wa chama cha matabibu kuwa jambo fulani lingetokea ambalo lingegonga vichwa vya habari kimataifa.
Upekuzi ulifanywa kwenye nyumba ya raia huyo wa Saudi Arabia mjini Stralsund ambaye ameishi Ujerumani kwa karibu miaka 20 lakini hakuna silaha zozote zilizopatikana. Katika tukio la pili, alimwandikia barua akimtishia mwendesha mashitaka mkuu wa serikali Agosti 15.