Nato hatimae yaafikiana
12 Julai 2018Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeafikiana juu ya suala tete la kuongeza kiwango cha bajeti ya ulinzi. Rais Donald Trump amesema nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo zimekubali kuongeza bajeti zao za ulinzi baada ya kufanyika kikao cha dharura katika siku ya pili ya mkutano wa kilele wa NATO mjini Brussels.
Rais Donald Trump amesema kwamba kila mmoja amekubali kutimiza ahadi zilizotolewa katika kiwango ambacho hakijapata kuonekana, lakini pia akasema Marekani inadhamiria kuiona Jumuiya ya NATO inabakia kuwa imara. Mkutano huo wa dharura leo uliitishwa baada ya Trump kutoa amri ya kutaka wanachama wote wa jumuiya hiyo waingize asilimia 2 ya pato jumla la nchi zao kwenye bajeti ya ulinzi akizishutumubaadhi ya nchi miongoni mwa wanachama 29 wa jumuiya hiyo kwamba hazitowi kiwango sawa na nchi nyingine katika jumuiya hiyo katika bajeti ya ulinzi. Awali rais huyo wa Marekani alitishia kuiondowa nchi yake katika jumuiya ya NATO lakini baada ya kufikiwa makubaliano amesema hakuna tena sababu ya kuchukua hatua hiyo:
"Niliwaambia watu kwamba sitofurahishwa hata kidogo ikiwa hawatotimiza ahadi kikamilifu kwasababu Marekani inalipa fedha nyingi pengine asilimia 90 ya gharama za NATO. Sasa watu wataanza kutimiza ahadi hiyo. kwahivyo hayo niliwaambia jana. Nilishangaa kwamba hayo hamkuyasema jana mnayasema leo. Lakini jana niliwaambia kwamba sifurahiswi kabisa na kinachotokea na wamezingatia kutimiza ahadi. Kwa hivyo sasa tunafurahishwa na tuko imara zaidi kama NATO, imara kuliko tulivyokuwa siku mbili zilizopita."
Trump, hata hivyo, hakufafanua ni nchi zipi zilizoahidi kutimiza ahadi ya kuongeza bajeti ya ulinzi na bado haifahamiki ikiwa nchi hizo zitabadili mipango yake. Nchi za Jumuiya hiyo zilikuabaliana 2014 kuelekea hatua ya kutumia asilimia 2 ya pato jumla la nchi zao katika bajeti ya ulinzi katika kipindi cha miaka 10 lakini NATO imekadiria kwamba ni wanachama 15 pekee au nusu ya idadi hiyo watakaoweza kumudu kiwango hichpo kufikia 2024.
Kansela Angela Merkel ambaye nchi yake imekosolewa zaidi na Trump katika suala la kuchangia kiasi kidogo katika bajeti ya ulinzi amesema Ujerumani na nchi nyingine pia katika Jumuiya hiyo ziko kwenye mkondo wa kuelekea kutimiza kile kilichopendekezwa na Trump:
"Rais wa Marekani amependekeza kile ambacho kimeshajadiliwa kwa miezi, kwamba suala la kugawana mzigo linabidi libadilike na sisi tumeweka wazi, mimi binafsi nimeweka wazi na wengine pia wamebainisha kwamba tuko katika njia ya kuelekea huko na kwamba hili ni suala la maslahi yetu wenyewe na hili litatufanya tuwe na nguvu.''
Kwa upande mwingine, Rais Emannuel Macron wa Ufaransa akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano huo ameonekana kuyapinga madai ya Rais Trump kwamba nchi zenye nguvu katika NATO zimekubali kuongeza zaidi ya kiwango cha asilimia 2 kilichokubaliwa mwanzo.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg pia amethibitisha juu ya nchi wanachama kuafiki hatua ya kuongeza bajeti ya ulinzi hadi asilimia 2 lakini ameshindwa kuthibitisha kile kinachodaiwa na Trump kwamba kiwango hicho kitaongezwa hadi asilimia 4.
Baada ya kuuwasha moto Brussels, Trump amekwenda Uingereza alikowasili mchana wa leo ambako pia awali alishamwaga mafuta ya petroli katika moto wa Brexit, masaa machache kabla ya kuwasili, kwa kusema kwamba hana hakika Waingereza waliupigia kura mpango wa Brexit uliowasilishwa na Waziri Mkuu Theresa May uliozusha mpasuko na uasi mkubwa katika baraza la mawaziri la Uingereza.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP/DPA/AFP
Mwandishi: Mohammed Khelef