NEW YORK: Wanawake wazidi kubaguliwa makazini
8 Machi 2007Leo ni siku ya wanawake duniani, ambapo umoja wa mataifa umesema kuwa pamoja na wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi , lakini wamekuwa wakilipwa ujira mdogo kulinganisha na wanaume.
Katika ripoti yake kuadhimisha siku hii ya wanawake duniani, Shirika la kazi la umoja wa mataifa ILO, limesema kumekuwa hali ya ubaguzi dhidi ya wanawake makazini.
ILO limesema kuwa wanawake wamekuwa wakilipwa mshahara mdogo ukilinganisha na wanaume kwa kazi inayofanana, na pia wamekuwa katika hatari zaidi ya kufukuzwa kazini..
Wanawake wanachukua idadi ya asilimia 60 duniani ya watu wanaofanya kazi duni, au wale wanaolipwa kiwango cha chini dola moja kwa siku.
Siku hii ya wanawake duniani iliwekwa na umoja wa mataifa mwaka 1977, kutambua mchango wa wanawake katika jamii.