1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni kina nani wagombea watatu wa Ukansela Ujerumani ?

Saleh Mwanamilongo
26 Septemba 2021

Kwenye uchaguzi wa Jumapili hapa nchini Ujerumani,vyama saba ndiyo vinapewa nafasi ya kupata viti Bungeni na vyama vitatu ndiyo vimesimamisha wagombea wa Ukansela.

https://p.dw.com/p/40sIg
Kombild Kanzlerkandidaten Triell | Laschet, Baerbock und Scholz

Ushindani mkubwa unatarajiwa baina ya vyama vitatu. Chama cha SPD na mgombea wake wa ukansela Olaf Scholz, mwenye umri wa miaka 63. Armin Laschet,aliye na miaka 60 kutoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU na mwanamama, Annalena Baerbock, mwenye miaka 40 aliyechaguliwa kuwa mgombea wa kwanza wa ukansela wa Chama cha Kijani.

 Armin Laschet mgombea wa chama cha CDU 

Armin Laschet ,mgombea ukansela wa chama cha CDU/CSU
Armin Laschet ,mgombea ukansela wa chama cha CDU/CSUPicha: Clemens Bilan/Pool/Getty Images

Kama ilivyo kwa Kansela Angela Merkel, Armin Laschet ni mwanachama chama cha kifahidhina cha Christian Democratic Union (CDU), ambacho ndiyo chama kikubwa zaidi katika bunge la Ujerumani, Bundestag.Armin Laschet ndiye waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani, la North Rhine-Westaphalia (NRW). Hali ambayo inaweza kumuwekea mazingira mazuri ya kufanikisha azma yake ya kuwa kiongozi mkuu ajaye wa Ujerumani.

Soma pia :Armin Laschet: Mgombea ukansela wa CDU

Wakati Laschet alipochaguliwa kama mwenyekiti wa chama mwezi Januari, wengi walimuona kama muungaji mkono mkubwa wa mwelekeo wa Merkel. Wakili huyo wa zamani na mwandishi habari - moja wa manaibu mwenyekiti watano wa CDU tangu 2012 - ameonekana kwa muda mrefu kama mtu wa karibu wa Merkel, pamoja na mrithi wake wa muda mfupi katika nafasi ya mwenyekiti, Annagret Kramp-Karrenbauer (2018 - 2020).

Mgombea Ukansela wa chama cha SPD

Olaf Scholz mgombea wa chama cha SPD
Olaf Scholz mgombea wa chama cha SPDPicha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake, mgombea wa chama cha SPD, Olaf Scholz anachukuliwa kuwa mwanachama wa tawi la kihafidhina la chama hicho, lakini pia ni mgumu kuhusishwa na matabaka ya kisiasa kama mrengo wa kushoto au mrengo wa kulia. Kama naibu kiongozi wa tawi la vijana la SPD la Jusos, mitizamano mingi ya Scholz ilikuwa mikali kijamii na inayokosoa vikali ubepari.

Soma pia: Mgombea ukansela wa Ujerumani kupitia SPD Olaf Scholz — Uhalisia juu ya nafsi

Sholz amefanya kazi kwa karibu na Merkel kama waziri wake wa fedha kwa zaidi ya miaka minne iliyopita na ndiye mgombea anayeongoza. Katika miezi iliyofuatia uteuzi wake kama kama mgombea mkuu, Scholz ameepuka kufanya makosa makubwa, na kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 15, chama chake cha SPD kimeupiku muungano wa vyama vya kihafhidhina vya CDU/CSU katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura.

Mgombea wa chama cha Kijani

 Annalena Baerbock kutoka chama cha Kijani
Annalena Baerbock kutoka chama cha KijaniPicha: Michael Kappeler/AFP/Getty Images

Mgombea mwengine anayefuatiliwa kwa karibu ni Annalena Baerbock kutoka chama cha Kijani. Baerbock mwenye umri wa miaka 40 aliibuka katika mkutano wa chama mapema 2018.

Mwanasiasa huyo wa jimbo ambaye hakuwa anajulikana sana -- mkazi wa jimbo la Brandenburg -- alisomea sheria mjini Hannover kabla ya kujiunga na chuo cha uchumi cha London, ambako alisomea sheria ya kimataifa. Matokeo yake, Baerbock anatoa mahojiano kwa Kiingereza fasaha -- jambo ambalo hadi katika wakati huu halichukuliwi kimzaha miongoni mwa wanasiasa wa Ujerumani.

Soma pia : Annalena Baerbock mgombea ukansela wa chama cha Kijani

Tangu aingie kwenye nafasi ya mwenyekiti mwenza wa chama hicho, Annalena amejitambulisha kama mtaalamu wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.