NICKEL MINES: Wasichana watatu wa shule wauwawa kwa kupigwa risasi
3 Oktoba 2006Polisi wa jimbo la Pennsylvania nchini Marekani wamesema mwanamume mmoja wa umri wa miaka 32 amewapiga risasi na kuwaua wasichana watatu baada ya kuwateka nyara katika shule ndogo ya jamii ya kidini ya Amish.
Wasichana wengine sita wamejeruhiwa katika kisa hicho wengine vibaya. Baadaye mwanamume huyo alijipiga risasi.
Shambulio hilo limefanywa baada ya onyo kutolewa kwa shule mbili za Nevada.
Rais George W Bush amehuzunishwa sana na kutatizwa na mauaji hayo. Amewaamuru maofisa wa serikali yake watafute njia za kukabiliana na mauaji katika shule.
Mauaji ya wasichana hao yanafuatia visa vyengine viwili vilivyotokea juma lililopita, ambapo msichana wa miaka 16 aliuwawa wakati mwanamume aliyekuwa na bunduki alipowateka nyara wanafunzi sita na kuwapiga risasi. Mwanamume huyo alijipiga risasi polisi walipokaribia kumkamata.
Mkuu wa shule ya upili ya Winsconsin aliuwawa kwa kupigwa risasi na mwanafunzi Ijumaa wiki iliyopita.