1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama azungumza na Brown kabla ya mkutano wa G20.

Sekione Kitojo1 Aprili 2009

Kabla ya mkutano wa kundi la mataifa ya G20 rais Barack Obama amekutana kwa mazungumzo hii leo na waziri mkuu Gordon Brown.

https://p.dw.com/p/HO7G
Rais wa Marekani Barack Obama, kulia na waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown wakati alipowasili namba 10 Downing Street mjini London kwa mkutano wao kabla ya mkutano wa G20.Picha: AP


Rais wa Marekani Barack Obama na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown wamekuwa na mazungumzo hii leo katika ofisi ya waziri mkuu katika mtaa wa downing katika mkesha wa mkutano wa kundi la mataifa ya G20 ili kuufufua uchumi wa dunia.


Obama na Brown wamekutana huku hali ya wasi wasi baina ya Marekani na bara la Ulaya kuhusiana na mapendekezo ya utawala wa rais Obama kwa ajili ya uratibu wa mipango ya dunia ya kichocheo cha uchumi ikitishia kuleta mgawanyiko mkubwa katika mkutano wa siku moja wa kundi la mataifa ya G20 unaotarajiwa kuanza kesho Alhamis.

Brown ambaye ni mwenyeji wa mazungumzo hayo, anakabiliwa na kazi ya kuziunganisha Marekani na Ulaya baada ya rais wa Ufaransa kusema kuwa rais Nicolas Sarkozy anaweza kutoka katika mkutano huo wa G20 iwapo hatakubaliana na utaratibu mkali katika sekta ya kifedha.

Wakati huo huo rais Nicolas Sarkozy na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanatarajiwa kukutana leo mchana mjini London kabla ya mkutano wa G20.

Rais Obama amewataka viongozi wote wanaohudhuria mkutano huo mjini London kulishughulikia suala hili kwa hali ya dharura.

Obama na mkewe Michelle, waliwasili jana Jumanne nchini Uingereza na kupokewa na mwenyeji wao waziri mkuu wa nchi hiyo Gordon Brown.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton pia aliwasili Downing Street pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza David Miliband muda mfupi baadaye.

Marekani inataka kuwapo mpango madhubuti wa uratibu wa kimataifa wa kichocheo cha uchumi katika mkutano huo wa G20 mjini London hapo kesho lakini inakabiliwa na mgawanyiko na nchi za Ulaya kama Ufaransa na Ujerumani, ambazo zinasisitiza utaratibu mzuri zaidi ili kuweza kupiga hatua.

Rais wa Marekani pia anatarajiwa kuwa na mazungumzo yanayosubiriwa kwa hamu kati yake na rais wa China Hu Jintao ambaye anakutana nae kwa mara ya kwanza. Baadaye Obama na mkewe wanatarajiwa kukutana na malkia Elizabeth ll pamoja na mumewe prince Philip kwa mara ya kwanza katika kasri la Buckingham.

Mji wa London utakuwa na maandamano siku nzima ya leo yatakayofanywa na waandamanaji wanaotaka mabadiliko makubwa katika nadharia za kibepari duniani kabla ya mkutano huo wa G20.

Likizo za polisi wote zimesitishwa na kiasi cha maafisa 10,500 wa polisi watatumika katika operesheni ya usalama katika mkutano huo wa G20.

►◄

Sekione Kitojo/RTRE

Mhariri Charo, Josephat.