Ocalan awataka wanamgambo kuacha mapigano Uturuki
1 Machi 2015Hii ni hatua muhimu katika kuelekea kumalizika kwa mapigano ya miaka 30 nchini Uturuki yanayoongozwa na waasi wa Kikurdi.
Rais wa Uturuki , Tayyip Erdogan, ameukaribisha wito huo lakini ametahadharisha kwamba waasi wameshindwa kutimiza ahadi zao za hapo kabla.
Sirri Sureyya Onder, mbunge katika chama cha Wakurdi cha Kurdish People's Democratic Party HDP, alisoma taarifa hiyo kutoka kwa Ocalan ambayo inakitaka chama cha Kurdistan Workers Party PKK kuhudhuria mkutano juu ya kuweka silaha chini katika miezi inayokuja ya machipuko.
Uamuzi wa kihistoria
"Nawaalika PKK kuhudhuria mkutano mkuu maalum katika miezi ya majira ya machipuko ili kutayarisha mikakati ya uamuzi wa kihistoria kuachana na mapambano ya silaha," Onder amesema , alimnukuu Ocalan, ambaye ujumbe wa chama cha HDP ulikutana nae wiki hii.
Onder alizungumza moja kwa moja katika matangazo ya televisheni pamoja na naibu waziri mkuu Yalcin Akdogan, ambae amesema hatua hiyo kuelekea kuweka silaha chini inaonesha " awamu muhimu katika hatua za kupata suluhisho imefikiwa," baada ya pande hizo mbili kukutana kwa muda mfupi mjini Istanbul.
"Tunaiona taarifa hii kuwa ni muhimu kuharakisha kazi ya kuweka silaha chini....na kwa siasa za kidemokrasia kujitokeza," Akdogan amesema.
Taarifa hiyo pia inaangalia hatua 10 za Ocalan ambazo Wakurdi wanataka kuhakikisha amani, ikiwa ni pamoja na katiba mpya ambayo Erdogan pia anaihitaji - na kuiweka ofisi yake na madaraka zaidi ya kiutendaji na kubadilisha katiba ambayo imetayarishwa na wataalamu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1980.
Erdogan alikabiliwa na hatari ya kupambana na wazalendo kwa kutafuta kumaliza mapigano ambayo yamesababisha zaidi ya watu 40,000 kuuwawa, wengi wao wakiwa Wakurdi, tangu mwaka 1984, na kuanzisha mazungumzo gerezani pamoja na Ocalan -- wakati fulani akionekana kuwa na kupewa jina la "muuaji wa watoto" -- mwishoni mwa mwaka 2012.
"Bila shaka miito ni mizuri, lakini kile kilicho muhimu ni utekelezaji. Ni kiasi gani utekelezaji utaakisi katika hali halisi kabla ya uchaguzi? Erdogan amesema katika mkutano na waandishi habari.
Ikikabiliwa na uchaguzi wa bunge mwezi Juni, serikali imesema inatarajia Ocalan kutangaza kumalizika kwa mapambano ya silaha ya kundi la PKK wakidai mamlaka zaidi ya haki za kitamaduni kwa Wakurdi wanaokadiriwa kufikia milioni 15.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sudi Mnette