Papa Benedikti alaani ndoa za jinsia moja
7 Juni 2005Vatikani:
Papa Benedikti XVI amelaani ndoa za watu wa jinsi moja , utoaji mimba na kupandikizwa mimba kwa njia za kitaalamu. Matamshi ya Kiongozi huyo mkuu wa kanisa katoliki duniani, yamekuja wakati wananchi wa Italia wakitarajiwa kupiga kura ya maoni Jumapili ijayo kuhusu suala la upandikizaji mimba kwa njia za kitaalamu. Papa Benedikti ameshambulia vikali kile alichokiita“uhuru wa vurugu“ wa mtindo wa kisasa wa watu wa jinsia moja kufunga ndoa. Makundi ya wasenge, wasagaji na jumuiya zao nchini Italia yanadai kwamba si kitisho kwa ndoa za kimaumile kati ya mwanamke na mwanamume. Tayari utaratibu wa watu wa jinsi moja kuowana umeruhusiwa katika nchi nyingi za Ulaya. Mnamo mwezi wa Aprili bunge nchini Uhispania ambayo kijadi ni nchi ya kikatoliki, kuliuidhinisha mtindo huo. Lakini bado hatua hiyo inapaswa kupitishwa na baraza la Senate kabla ya kuwa sheria.