Rais Ruto: Kenya haitokwepa kulipa madeni yake
5 Januari 2023Matangazo
Akizungumza katika mahojiano na vyombo vya habari vya ndani vya Kenya, Ruto amesema taifa hilo halitashindwa kutimiza wajibu wake wa kulipa madeni na hivi sasa wamechukua hatua ya kuweka vizingiti kwa serikali kupata mikopo mipya.
Serikali ya Ruto, ambayo ilichukua hatamu mwezi Septemba, imesema inapanga kupunguza ukopaji wa gharama kubwa wenye masharti ya kibiashara na badala yake kutumia taasisi zenye masharti nafuu kama Benki ya Dunia ili kupunguza shinikizo la ulipaji wa deni la taifa.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoinukia kiuchumi, Kenya ilikaribia kushindwa kupata fedha kutoka kwa masoko ya kimataifa ya mitaji mwaka 2022 kutokana na kupanda kwa kiwango cha riba kwenye mauzo ya amana mpya za serikali.